• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
MUME KIGONGO: Wanaume wenye kiwewe hatarini kuugua maradhi ya moyo, kisukari

MUME KIGONGO: Wanaume wenye kiwewe hatarini kuugua maradhi ya moyo, kisukari

NA CECIL ODONGO

WANAUME wa umri wa kadri ambao hushikwa na wasiwasi mwingi wako katika hatari ya kupata ugonjwa wa moyo, kiharusi na kisukari, utafiti umebaini.

Watafiti kutoka Chuo cha Harvard Marekani, wamegundua kuwa mwanaume akiwa na wasiwasi mara nyingi kuhusu changamoto mbalimbali, basi yupo katika hatari ya kupata magonjwa hayo mapema sana wakati wa uhai wake.

Hii ni kinyume na wanaume ambao huchukulia changamoto kama suala la kawaida, kupuuza baadhi yake na kutokuwa na wasiwasi. Ni nadra sana kupatwa na magonjwa haya hatari iwapo mwanaume hana wasiwasi.

“Kuwa na kiwango cha juu cha wasiwasi huongezea kwa asilimia 10 hadi 13 kuwa na magonjwa ya moyo, kiharusi na kisukari,” ikasema sehemu ya ripoti kwenye jarida moja la kiafya chuoni humo.

Kwa kawaida, Wanasayansi wamekuwa wakikisia kuwa magonjwa hayo huchangiwa na tabia kama uvutaji sigara, uraibu wa kunywa pombe au matumizi ya dawa nyingine za kulevya.

Mwanzo, wasiwasi mwingi huchangia mabadiliko hasi ya kibayolojia ndani ya mwili ambayo huongeza mpigo wa moyo na kupanda kwa shinikizo la damu. Kuna wanaume ambao kutokana na maumbile, makuzi na malezi yao, hutokea kuwa na mazoea ya kuandamwa na wasiwasi hata kuhusu masuala madogo.

Watafiti sasa wanapendekeza kuwa, mtu anastahili kujizuia kuwa na wasiwasi mara kwa mara kwa kushiriki mazoezi mara kwa mara na kupata usingizi wa kutosha.

Pia, wanashauri kuwa ni muhimu kujizuia kunywa pombe na kupata ushauri kuhusu mambo yanayokutatiza na kusababisha wasiwasi mwingi.

  • Tags

You can share this post!

Acha kunipa presha, Ruto amfokea Raila

Arsenal wachapa West Ham na kupepea zaidi kileleni mwa...

T L