• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Mzozo wa DPP na IPOA kuhusu askari watundu

Mzozo wa DPP na IPOA kuhusu askari watundu

NA MWANGI MUIRURI
NJAMA mpya za kuwakinga maafisa wa polisi watukutu kutoka kwa mashtaka mahakamani imezinduliwa, huku kukitolewa taarifa kesi zote kuwahusu ziwe zikiwasilishwa kwa makao Makuu ya Mkurugenzi wa Mashtaka (ODPP) ili kupewa mwelekeo.

Kupitia barua rasmi kutoka kwa ODPP ikiwa na sahihi ya Naibu Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Bw Victor Mule, utaratibu sasa wa kushughulikia kesi dhidi ya maafisa wa polisi unafaa kuanzia kwa tume huru ya kupiga msasa utendakazi wa polisi (IPOA), lakini uamuzi wa mwisho kuhusu mashtaka udhibitiwe.

Wakati IPOA iliundwa na katiba ya 2010, ilipewa uwezo wa kuchunguza maafisa wa polisi na kupendekeza mashtaka bila ya mwingilio wowote, licha ya kuwa nayo afisi ya DPP ndiyo imetwikwa mamlaka huru ya kuidhinisha kesi kuzinduliwa mahakamani hivyo basi kuzua mgongano wa taasisi hizo mbili.

“Baada ya IPOA kukamilisha uchunguzi wao, faili zitakazoandaliwa zinafaa kuwasilishwa kwa ODPP ili mwelekeo wa kushtaki au kuachana na kesi hizo utolewe,” barua hiyo inaelezea.

Bw Mule ameelekeza kwamba barua hiyo inakiliwe viongozi wote wa mashtaka nyanjani ili wajifahamishe na mwelekeo huo mpya.

Aidha, Mule katika ujumbe huo ameelezea kwamba idhini ya kushtaki maafisa wa polisi inafaa kusakwa kutoka makao makuu ya ODPP wala sio kwa afisi za nyanjani.

Maafisa wa polisi wamekuwa wakielezea wasiwasi wao na uhuru wa IPOA, wengine wakiteta kwamba kuna mikakati ya kikazi tume hiyo haielewi na huwa inapendekeza maafisa waadhibiwe kwa kutekeleza miradi ya kufaa nchi.

“Hatukatai kwamba tuna maafisa watundu ambao hutekeleza majukumu yao dhidi ya raia kwa njia ya kihuni na ujambazi. Lakini kuna wengine wengi ambao hutekeleza majukumu rasmi na spesheli kwa niaba ya vitengo vyote vya kiusalama na kwa niaba ya serikali kwa ujumla,” akasema afisa mmoja wa ngazi ya juu.

Alidokezea Taifa Leo Dijitali kwamba “kuna miradi ya kuangamiza maadui wa taifa na ambayo huwa imeamrishwa na kamati kuu ya kiusalama na ambayo mwenyekiti huwa ni rais aliye mamlakani akisaidiana na viungo vingine muhimu vya kudhibiti usalama wa kitaifa”.

Afisa huyo alisema kwamba IPOA hutekeleza majukumu yake kana kwamba maafisa wa usalama ni waumini katika kanisa fulani ambao hudhibitiwa na maandiko matakatifu chini ya amri za kitabu cha dini.

“Kuna mauaji ambayo tupende tusipende ni lazima yatokee dhidi ya wahalifu sugu…Ni lazima wengine wakabiliwe kwa fujo…Uhuru kwa majambazi ni machozi kwa taifa na watu wake…Kuadhibu maafisa ambao wametekeleza uzalendo wa kuokoa nchi kupitia maangamizi au fujo dhidi ya wahalifu hao sugu ni sawa na kusaliti nchi,” akasema, akiongeza kuwa “hii ndiyo hali wengi ndani ya IPOA hawaelewi wanapokimbizana na kesi dhidi ya polisi”.

Suala hili limezua hisia kali huku majaribio yetu ya kupata maoni ya Mwenyekiti wa IPOA Bi Anne Makori yakigonga mwamba.

Lakini duru ndani ya IPOA zilisema kwamba “tutangojea kuzuke hali moja ambapo tutakadiria maafisa watukutu wanakingwa dhidi ya kuwajibikia sheria ndipo tujieleze kikamilifu”.

Afisa mmoja katika bodi ya IPOA alisema kwamba “kumekuwa na majaribio tele ya kuhujumu IPOA kupitia hata kubuniwa kwa kitengo sambamba ndani ya polisi kwa jina Internal Affairs Unit (IAU) cha kuchunguza maofisa walioshukiwa kukiuka sheria”.

Aliongeza kwamba “kumekuwa na matamshi kutoka kwa wakuu wa kiusalama ambao wametuita wapuuzi na wasiojielewa kama njia moja ya kutuhujumu”.

Afisa huyo alisema kwamba “sisi tutaendelea kutekeleza majukumu yetu kwa mujibu wa sheria na tupendekeze watundu washtakiwe ili mkurugenzi wa mashtaka ya umma akikataa, tujue hujuma imefanywa rasmi na tutateta washangae”.

Maafisa wengine wamekuwa wakitaka mabadiliko pana ya mikakati, pendekezo likiwa kuundwe mahakama kama ya jeshi ya kushtaki maafisa wa polisi.

Wamekuwa wakiteta kwamba kuwakamata maafisa wa polisi na kuwafungia seli moja na raia pamoja na kuwapeleka rumande na jela ambako kumejaa raia waliokamatwa na maafisa haohao ni hatari sana kwa maisha yao.

“Tunafaa kukamatwa na kuwasilishwa kwa mahakama spesheli ya polisi ambapo kesi zikisikizwa na kuamuliwa, wa kufungwa afungwe katika taasisi maalum ya polisi kwa kuwa hata kutuweka seli na jela za kawaida kuna hatari kwa kuwa tunaweza tukawaelimisha wafungwa jinsi ya kukwepa mitego ya ushahidi wa kesi, tutoe siri za polisi na pia tuwape mafunzo hata ya silaha,” akasema afisa mmoja.

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Hayawi hayawi…Jackie Matubia afichua mchumba wake mpya  

Taulo za hedhi zilizotumika zazidi kuwa kero mitaa kadha...

T L