• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Taulo za hedhi zilizotumika zazidi kuwa kero mitaa kadha Nairobi   

Taulo za hedhi zilizotumika zazidi kuwa kero mitaa kadha Nairobi  

NA SAMMY WAWERU

WAKAZI kutoka mitaa kadhaa Kaunti ya Nairobi wanalalamikia kuendelea kutapakaa kwa taulo za hedhi na nepi za watoto.

Taulo za hedhi, ni bidhaa maalum zinazotumiwa na wanawake nyakati zao za mwezi ambazo huhusishwa na utokaji damu.

Nepi nazo, hufungwa watoto wachanga sehemu nyeti ili kusitiri haja; mkojo na kinyesi.

Licha ya manufaa ya bidhaa hizo, zimegeuka kuwa kero Nairobi zikitupwa kiholela kwenye majaa ya taka.

Kwa mfano, katika mtaa wa Zimmerman, Roysambu, Kasarani na Mwiki, zinaendelea kutapakaa jambo ambalo linazua wasiwasi kwa wenyeji.

Jaa lenye taulo za hedhi na nepi za wa watoto katika mtaa wa Zimmerman, Nairobi. PICHA|SAMMY WAWERU

Hata ingawa wao wenyewe ndio wakaazi, baadhi wanalalamikia taulo hizo za hedhi na nepi kujaa kila mahali.

“Kila jaa la taka na kando kando mwa barabara, zimetapakaa,” Phaustine Omutere, mkaazi mtaa wa Zimmerman akaambia Taifa Leo Dijitali. 

Mbali na Zimmerman, Roysambu, Kasarani na Mwiki, mitaa mingine iliyoathirika ni Githurai, Kahawa West, Kahawa Wendani na Sukari, Mathare, Kariobangi, na ile ya mabanda.

Hali ni mbaya kiasi kwamba bidhaa hizo zilizotumika zinarushwa nyuma ya nyumba za kukodisha.

Nepi ya mtoto kwenye jaa. PICHA|SAMMY WAWERU

Zinaibua hatari ya usalama wa mazingira.

“Ni chocheo la mkurupuko wa maradhi hatari yanayohusishwa na mazingira,” akasema Esther Mbabu, mwenyeji Zimmerman.

Katika mtaa huohuo, kwa mfano, kila barabara unayopotia hutakosa kuona taulo za hedhi na nepi.

Kinachozua hofu zaidi ni kwamba zimetumika, zingine zikiwa wazi hedhi inaonekana na haja.

“Ndio, zinatufaa ila kwa watoto wachanga wanaochezea nje bila kutofautisha majaa na uga ni hatari kwao,” Simon Muturi, mkaazi Kahawa West akaelezea.

Ni hali ambayo endapo haitadhibitiwa, huenda ikasababisha mkurupuko wa magonjwa kama vile Kipindupindu na Homa ya Matumbo, ikizingatiwa kuwa bidhaa hizo pia zinatupwa kwenye mitaro yenye mifereji ya kusambaza maji.

Kulingana na malandilodi na keateka wa majengo ya kukodi, kila ploti ina mikakati ya ukusanyaji taka.

Aidha, kuna wahudumu waliojukumika kukusanya taka kila wiki.

“Aghalabu, hutoza ada ya Sh200 kila mwezi kwa kila mpangaji na taka hupelekwa mahali salama dhidi ya mazingira,” anasema Benson Mwangi, keateka Roysambu.

Taulo ya hedhi iliyotumika kwenye jaa la taka na nepi zenye kinyesi. PICHA|SAMMY WAWERU

Samuel Kamau, mmoja wa wahudumu wa kampuni zinazokusanya taka Thika Road anasema baadhi ya wapangaji inakuwa vigumu kuwashinikiza kutoa malipo.

“Kuna wanaopanda juu ya majengo na kutupa taka kiholela. Muhimu ni serikali iwachukulie sheria na hatua za kinidhamu ili kampeni kudumisha usafi wa mazingira iafikike,” Kamau akapendekeza.

Taifa Leo Dijitali, imezuru baadhi ya mitaa na kubaini fika kuwa taulo za hedhi na nepi za watoto zinaendelea kutapakaa kwenye majaa ambayo yanajitokeza kinyume na inavyopasw.

Mamlaka ya kitaifa kusimamia mazingira, ndiyo NEMA, inawajibika kwa utepetevu kama unaoshuhudiwa mitaa iliyoathirika.

Ni wajibu wa taasisi hiyo ya kiserikali kuonyesha makali yake kwa wahusika.

Mojawapo ya jaa mtaani Zimmerman ambalo limegeuka kuwa eneo la kutupwa taulo za hedhi na nepi za watoto zilizotumika. PICHA|SAMMY WAWERU
  • Tags

You can share this post!

Mzozo wa DPP na IPOA kuhusu askari watundu

Wandayi: Dosari za KCPE huenda zikaibuka kwenye KCSE  

T L