• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:55 AM
Ndindi Nyoro: Wakosoaji wa Ruto wamefanyia Kenya nini?

Ndindi Nyoro: Wakosoaji wa Ruto wamefanyia Kenya nini?

NA SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Kiharu, Ndindi Nyoro ameendeleza mashambulizi yake kwa wakosoaji wa Rais William Ruto akiwataka waainishe maendeleo waliyoletea nchi. 

Akionekana kulenga muungano wa Azimio la Umoja, Bw Nyoro amesema vinara wanaoongoza mrengo huo wamekuwa kwenye serikali hapo awali na angetaka waorodheshe maendeleo waliyofanya.

Azimio inaongozwa na Bw Raila Odinga, ambaye amewahi kuhudumu kama Waziri Mkuu – Chini ya utawala wa serikali ya Rais mstaafu Hayati Mzee Mwai Kibaki.

Ndindi Nyoro, ambaye ni mwandani wa Rais Ruto, anasema upinzani una haki Kikatiba kukosoa serikali ila kwa njia ya heshima.

“Tunawahimiza kwa njia ya heshima, waendelee kufanya kazi ya upinzani vizuri – Kukosoa serikali. Hata hivyo, kwa wale ambao wamekuwa kwenye serikali za hapo awali, mnapokosoa serikali mjiulize ni nini mmewahi kufanyia Kenya,” mbunge huyo wa chama tawala cha UDA akasema.

Huku Azimio ikishinikiza serikali ya Kenya Kwanza kupunguza gharama ya maisha, hasa kushusha ushuru (VAT) unaotozwa bidhaa muhimu za kimsingi, Bw Nyoro anasema si haki kwa upinzani kupaka Dkt Ruto matope ilhali amekuwa mamlakani chini ya mwaka mmoja na nusu pekee.

“Kwa wale ambao mmekuwa serikalini kwa muda wa miaka 10, ni maendeleo yepi hasa mmefanya? Tunapoibua malalamishi, tuwe wenye haki,” Mwenyekiti huyo wa Bajeti Bungeni akasema kupitia video.

Akaongeza, “Tumpe Rais wetu muda afanye kazi, tumheshimu na zaidi ya yote tumuombee Mungu amsaidie afaulu”.

Mbunge huyo mcheshi alidai kwamba baadhi ya viongozi upinzani wanahangaisha serikali ikiwa kama njia mojawapo kumuwekea Dkt Ruto mitego ili “aanguke”.

Upinzani unaitaka serikali ya Rais Ruto kupunguza ushuru, hasa kwa mafuta ya petroli.

Mwaka huu, 2023, Ruto alipandisha VAT ya bidhaa za petroli kutoka asilimia 8 hadi 16.

Nyongeza hiyo imechochea bidhaa nyingi za kimsingi kupanda bei, ikizingatiwa kuwa mfumko wa mafuta ya petroli unaathiri sekta ya uchukuzi na usafiri kwa kiwango kikubwa.

  • Tags

You can share this post!

Ambia Samidoh akujengee boma lako, Karen Nyamu aambiwa

Pepo wa mauti alivyotembelea Murang’a  2023

T L