• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 1:05 PM
NDIVYO SIVYO: Upambanuzi wa kina wa kama, kamua na suuza

NDIVYO SIVYO: Upambanuzi wa kina wa kama, kamua na suuza

Na ENOCK NYARIKI

SHABAHA yetu katika makala ya awali ilikuwa kutofautisha baina ya maneno kama na kamua ambayo aghalabu hutumiwa visivyo.

Hata hivyo,katika kulijadili jambo hilo, tulikumbana na utata mwingine unaolizunguka neno kama.

Baadhi ya watu hupinga matumizi yake kuonyesha kuwa hali, mtu au kitu kina sifa, wadhifa au matumizi sawa na kingine au mwingine. Neno ‘kuwa’ hupendekezwa kutumiwa ili kuibua maana ya kijelezi tulichokitaja hapa juu. Neno hili la pili linadhaniwa kuwa na maana sawa na kitenzi kishirikishi kipungufu {ni}.

Tutaziangazia sentensi mbili tulizozitaja ili kuonyesha kwa nini neno kuwa haliwezi kufidia nafasi ya ‘kama’ mia fil mia. Matumizi ya ‘kuwa’ katika sentensi ya (b) yanaifanya kuwa na maana tofauti kabisa na ile ya (a) au hata kutatiza maana inayokusudiwa. Matumizi ya ‘akiwa’ kwa maana hiyo yaani ‘alitoa amri akiwa kamanda wa polisi’ hayatasaidia kutatua utata tulioutaja kwa sababu neno hilo pia si ‘kufu’ ya kama.

Neno kama linapotumiwa kama kitenzi, huibua maana ya kuminya chuchu za mnyama kwa mfano ng’ombe ili maziwa yatoke. Nitairejelea maana hii baadaye ila ni muhimu kwanza kuiangazia maana ya neno ‘kamua’. Shangazi yangu hulitumia neno kamua kwa maana ya kuviosha vyombo au nguo kwa maji safi ili kuondolea mbali povu.

Shangazi, pamoja na watu wengine katika tapo lake hudhani kuwa ‘kukamua’ ni kusafisha tena kwa maji safi kwa nia ya kutakasa. Neno ‘kukamua’ lina maana ya kukibinya kitu ili kuondoa uowevu ulio ndani yake. Mfuaji nguo anapotaka kuondoa povu kwenye nguo anazisuuza ilhali akitaka kuondoa maji kwenye nguo zenyewe kabla ya kuzianika pengine kwa kutaka ziamae haraka huzikamua.

Alhasili, ipo tofauti kati ya neno ‘kamua’ na ‘kama’. Iwapo dhamira ya mzungumzaji ni kueleza kitendo cha kutoa maziwa katika chuchu za mnyama kwa kuminya, neno mwafaka linalopaswa kutumiwa katika mazingira hayo ni kukama.

Iwapo lengo ni kuelezea utoaji wa uowevu, kwa mfano maji kwenye nguo, tunatumia kamua. Kwa hivyo,kitenzi ‘kamua’ kisitumiwe kwa maana ya kuzitakasa nguo kwa maji safi.

Neno mwafaka linalopaswa kutumiwa kwa fasili hiyo ni kusuuza. Hata hivyo, kuna neno sunza ambalo ni kitate cha suuza. Hili lina maana ya kupapasa kwa mkono au mguu gizani ili kutafuta kitu au kutambua unapoelekea. Maana yake ya pili ni kuleta usumbufu au kero n.k.

You can share this post!

Jubilee yacheza ngware chaguzi ndogo

USWAHILINI: Si kila paka mweusi Pwani ni jini, lakini…