• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 9:48 PM
USWAHILINI: Si kila paka mweusi Pwani ni jini, lakini…

USWAHILINI: Si kila paka mweusi Pwani ni jini, lakini…

Na HAWA ALI

MJI wa pwani wa Mombasa umejaa maonyesho ya asili yenye kuvutia ajabu.

Jamii za wenyeji zinajulikana kuwa karimu na mara nyingi zinakaribisha sana watu. Mji huu una historia inayojulikana, kuwa asili ya “majini”. Hawa ni viumbe wa kiroho ambao huzunguka jiji kwa njia mbalimbali.

Inaaminika kwamba wageni wanaozuru pwani hawapaswi kuwabughudhi au kupigapiga paka wanaokutana nao, au hata kumshirikisha kwa njia yoyote.

Karibu na eneo la Mtopanga mmiliki wa nyumba alilazimika kuondoka kwenye eneo lake baada ya kuteswa bila kuchoka na viumbe asiowaona. Hatimaye aliondoka nyumbani, lakini aliweka mtego ili kupata kujua kiini cha dhiki zake. Kiini ama asili ya viumbe hawa wa ajabu.

“Nilijipa ujasiri na kujaribu kumtoa paka kutoka kwa mtego na kugundua tu kwamba kichwa chake kilikwama katika shimo dogo la mtungi niliokuwa nimeuweka kama mtego,” anasema Hamisi, mzee wa kijiji cha Mtopanga, Timboni.

Mwishowe paka alifanikiwa kutoka ingawa idadi ya watu waliokuja kumshuhudia akiwa ameshikwa kwenye mtungi huo ilikuwa inaongezeka.

Mzee Hamisi, anasema kuwa baada ya kutoweka kwa paka na kifo cha mwanamke mzee anayeishi karibu na nyumba hiyo, na ambaye alishukiwa kuwa mchawi, matukio ya pesa kutoweka majumbani, maduka na kabatini yalimalizika ghafla. Wenyeji waliamua kuita mahali hapo, Stage ya Paka.

Hadithi za ajali karibu na eneo la Kibarani zote zinafanana. Madereva wanadai kuwa wameona paka akipita barabarani na wanapopunguza mwendo kasi, paka hubadilika kuwa mwanamke mrembo na ajali hutokea.

Wafanyabiashara nao walilalamika kuhusu jinsi mambo yalivyozidi kuwa mabaya wateja wanapoanza kususia maduka yao.

“Kila siku, mara tu baada ya kufungua duka langu, paka alikuja na kusimama nje ya duka, akinitazama na kuondoka. Baada ya hapo, singefanya mauzo yoyote, ”anasema Mama Ciro, ambaye wakati mmoja alikuwa na duka huko Migadini.

Paka hao ambao wengi wao ni wenye rangi nyeusi sana wamezidisha hofu kwa baadhi ya wakazi na wafanyabiashara, huku wengi wakichagua kutowasumbua hata wanapowaona wakishambulia kuku wao.

“Niliwahi kuona paka akifukuza kuku. Niliingilia kati na kumfukuza paka lakini mara ghafla aligeuka na kunikabili. Niliondoka nikiwa na hofu, ”Juma Rashid, ambaye anaishi Mwandoni anasema.

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Upambanuzi wa kina wa kama, kamua na suuza

Guardiola ataka Manchester City kujinyanyua upesi na...