• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
NGUVU ZA HOJA: Ikiwa Sheng ni kizawa cha Kiswahili, Shembeteng ni mjukuu wa Kiswahili?

NGUVU ZA HOJA: Ikiwa Sheng ni kizawa cha Kiswahili, Shembeteng ni mjukuu wa Kiswahili?

NA PROF IRIBE MWANGI

JUZI nikipitapita mjini, nilikutana na vijana wawili wakizungumza kwa lugha ambayo niliiona kwamba naielewa lakini ambayo hakika sikuielewa.

Nilipowauliza hiyo ilikuwa Sheng ipi waliyoitumia, mmoja alinijibu kwamba lugha waliyoitumia haikuwa Sheng ila “kizalia cha Sheng kiitwacho Shembeteng.”

Sikuelewa na kwa hivyo niliazimia kudadisi zaidi. Niliarifiwa kuwa kwa mujibu wa waasisi wake wanaojiita Jeshi Jinga, Shembeteng ina viambishi ndani vitano, yaani, mbata, mbete, mbiti, mboto na mbutu.

Viambishi hivi huongezwa baada ya silabi ya pili kutoka mwisho wa neno, mfano, wangu huwa inakuwa wambatangu, kiti ni kimbititi, shona ni shombotona na jua jumbutua. Irabu ya silabi hiyo ya pili kutoka mwisho huamua kiambishi kitakachotumiwa na hivyo urari huzingatiwa.

Shembeteng haijikiti tu katika Kiswahili bali pia Kiingereza na hata Sheng. Kwa mfano, neno nakulombotov linatokana na nakulove ambayo ni Sheng inayochanganya Kiswahili na Kiingereza. Silabi ya pili kutoka mwisho inaisha kwa irabu -o na hivyo kiambishi mboto ndicho kinachochopekwa na kuzaa neno nakulombotov.

Swali ni je, Shembeteng ni lugha? Je, Itaweza kusambaa kimatumizi kama vile Sheng? Je, matumizi yake yana athari gani kwa ujifunzaji na utumiaji wa Kiswahili Sanifu?

Ni muhimu wadau wote wayajadili maswali haya. Kuyafumbia macho masuala ya kiisimujamii kama haya huenda yakazua tatizo kubwa katika ufunzaji na usambazaji wa Kiswahili. Ushawishi wa vijana wanaoibuka na lugha au vijilugha au misimbo kama hii, hauwezi kupuuziliwa mbali.

You can share this post!

USHAURI NASAHA: Yajaze mazingira yako uchangamfu ili ufuzu...

NGUVU ZA HOJA: Umuhimu wa maadhimisho ya Siku ya Kiswahili...

T L