• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
NJENJE: Kenya yapunguza uagizaji sukari uzalishaji ukiongezeka

NJENJE: Kenya yapunguza uagizaji sukari uzalishaji ukiongezeka

NA WANDERI KAMAU

KENYA ilipunguza uagizaji sukari kwa nusu mnamo Juni ikilinganshwa na mwezi Mei, baada ya uzalishaji miwa kuongezeka kwa asilimia 11 nchini.

Maelezo kutoka Idara ya Kusimamia Sukari Kenya (SDK) yanaonyesha kuwa kiwango cha sukari ambacho Kenya iliagiza kutoka nje kilipungua kutoka tani 50,881 mnamo Mei hadi tani 33,650 mwezi Juni.

Idara hiyo ilisema kuwa uzalishaji wa sukari uliongezeka kwa asilimia 11.3 hadi tani 70,376.

Kiwango hicho ndicho cha juu zaidi cha sukari kuzalishwa tangu Januari 2022.

Ongezeko la uzalishaji wa bidhaa hiyo umechangia bei yake kubaki chini, ikilinganishwa na bidhaa nyingine.

Kwa sasa, kilo moja ya sukari inauzwa kwa Sh128, ikilinganishwa na Sh129 mnamo Mei.

Wafanyabiashara wamekuwa wakiuza paketi ya kilo mbili ya sukari kwa Sh239 kiwastani.

“Kijumla, uzalishaji wa sukari Juni ulikuwa tani 70, 376 ikilinganishwa na mwezi uliotangulia, ambapo Kenya ilizalisha tani 63, 209,” ikaeleza idara hiyo kwenye ripoti yake.

Katika viwanda vya sukari, bei ya gunia moja la zao hilo ilishuka kutoka Sh5,261 mwezi Mei hadi Sh5, 199 mwezi Juni.

Hilo linaonyesha athari za kuongezeka kwa uzalishaji wake katika miezi ya hivi karibuni, ikilinganishwa na hapo awali.

Mnamo Aprili, Kenya iliagiza tani 21, 665 za sukari. Kiwango hicho kiliongezeka na kufikia tani 33, 650 mnamo Mei.

Kenya ililazimika kuongeza kiwango hicho kutokana na kupungua kwa miwa iliyosagwa. Kijumla, viwanda vya sukari vilisaga jumla ya tani 673, 197 ya miwa, ikilinganishwa na tani 719,481 mwezi uliotangulia.

Kupungua kwa miwa iliyosagwa mnamo Mei kulichangia sukari iliyozalishwa nchini kupungua kwa asilimia nane hadi tani 63, 209.

Kenya imeruhusiwa kuagiza hadi tani 350,000 za sukari kutoka kwa mataifa wanachama wa Jumuiya ya COMESA.

Wasagaji wa sukari nchini wamekuwa wakilalamika kuwa serikali imekuwa ikiruhusu uagizaji wa sukari nyingi kuliko kiwango ambacho Kenya inahitaji.

You can share this post!

MITAMBO: Kifaa kinachosaidia kuboresha rutuba

UJASIRIAMALI: Ukakamavu umemuinua katika uuzaji wa mitumba

T L