• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 10:55 AM
MITAMBO: Kifaa kinachosaidia kuboresha rutuba

MITAMBO: Kifaa kinachosaidia kuboresha rutuba

NA RICHARD MAOSI

MKULIMA anaweza kuendesha kilimo kwa kutumia jembe lenye ncha kali kulima kati ya mseto wa mimea ingawa jembe la kawaida haliwezi kupenya hadi kufikia udongo wenye kina kirefu.

Hata hivyo, teknolojia za kuendesha mabadiliko ya mbinu za kilimo zipo tele mojawapo ikiwa ni mtambo wa patasi ya kilimo almaarufu kama chisel plough, uliovumbuliwa ili kurahisisha shughuli za kulima, hususan wakati wa kuandaa shamba kabla ya msimu wa kupanda.

Kulingana na Douglas Mburu kutoka wizara ya Kilimo Kaunti ya Nakuru, utekelezaji wa kilimo endelevu unahitaji kuelewa mbinu za kilimo na athari zake kwa malighafi asilia.

Mtambo wenyewe ni wa manufaa katika karne hii ambayo wakulima wanahimizwa kuendesha kilimo kidijitali ili kuboresha mazao yanayovunwa kila msimu na vilevile husaidia kupunguza gharama ambapo mkulima hutumia hela nyingi kuwaajiri vibarua.

Mburu anasema kupitia matumizi ya mtambo huu, mfumo mzima wa ikolojia unaweza kustawika, kwa sababu hutoa mazingira mazuri ya kuwavutia wadudu muhimu aina ya nyungunyungu ambao husaidia kuimarisha kiwango cha virutubisho ndani ya mchanga.

Mtambo wa Chisel plough ambao hutumika kuendesha kilimo cha kina kirefu. PICHA | RICHARD MAOSI

Anasema kuwa katika hatua za kupanda, wakulima wengi wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi hasa pale wanapotumia jembe la mkono kutengeneza mashimo ya kupanda mbegu.

“Izingatiwe kuwa mkulima anatakiwa kwanza kulainisha udongo kabla ya kufukia mbegu zake ili kutoa fursa kwa hewa safi na unyevu kupenya baina ya mchanga na kufikia mimea,” asema.

Kwa kawaida matumizi ya jembe la mkono huchukua muda mrefu kukamilika na hivyo, mazao huchukua wakati mrefu kuchipuka, kustawi na kukomaa.

Mburu anaeleza kuwa mtambo wa chisel plough hutumika kuvunja vipande vya udongo na kupindua mchanga, hali ambayo husaidia kuondoa masalio ya visiki na magugu shambani.

Kwa kutumia kifaa hiki, masalio yanaweza kuondolewa kabisa shambani ama kusongezwa pembeni na hata kuchanganyika na udongo ikiwa ni njia mojawapo ya kutengeneza rutuba.

“Kifaa chenyewe kinaweza kukokotwa na mnyama kama vile fahali au trekta na mara nyingi hutumika katika sehemu ambazo mkulima anaendesha kilimo katika kipande kikubwa cha ardhi, kwa mimea kama vile mkonge, mahindi, ngano, mtama na mpunga,” anaeleza.

Anawashauri wakulima kutoka maeneo kame sehemu ambazo huwa zimejaa mawe kiasi kwamba mizizi ya mimea haiwezi kupenya ardhini, kukumbatia kifaa hiki.

“Matumizi ya kifaa hiki huwa ni mepesi ikizingatiwa kuwa baada ya kubandikwa katika trekta, huanza kukokotwa,” anaeleza.

Mtambo wa chisel plough huanza kuzunguka na kuweka shinikizo katika ardhi.

Mtambo wenyewe huwa umetengenezwa kwa chuma na kuchukua umbo la mstatili, ambapo udhabiti wake husaidia kifaa chenyewe kupenya ardhini.

Aidha, aliongezea kuwa mtambo wenyewe unaweza kupenya hadi sentimita 40 ardhini, hali ambayo husaidia kutengeneza njia mbadala kwa michirizi ya maji kupenya.

Kwa upande mwingine, Naomi Chemain ambaye ni mhandisi kutoka wizara ya kilimo, anasema mtambo wa chisel plough unaweza kumsaidia mkulima kutunza hadi asilimia 40 ya unyevu unaopatikana kwenye mchanga.

“Pia kiwango cha mimea kuota huongezeka baina ya asilimia 15-20,” anaongeza.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Asema kilimo kinalipa bora hatua zinazofaa...

NJENJE: Kenya yapunguza uagizaji sukari uzalishaji...

T L