• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
OFAB yatuza wanahabari walioripoti vyema mfumo wa bioteknolojia kuboresha kilimo

OFAB yatuza wanahabari walioripoti vyema mfumo wa bioteknolojia kuboresha kilimo

NA SAMMY WAWERU

WANAHABARI wa Kenya ambao wameonyesha umahiri katika kuripoti matumizi ya mfumo wa Bioteknolojia kwenye kilimo wametuzwa.

Wamezawadiwa kufuatia makala ya kuelimisha yaliyochapishwa kati ya Agosti mwaka ulioipita, hadi Agosti mwaka huu.

Shirika linalohamasisha Matumizi ya Bioteknolojia kwenye Kilimo (OFAB-Kenya), limetambua jitihada zao likihimiza vyombo vya habari kuendelea kuipa kipaumbele teknolojia na mifumo ya kisasa kuboresha shughuli ya kilimo.

Linashirikisha utangamano wa Wanasayansi, wanahabari, mashirika ya kijamii kutetea haki za kibinadamu, wenye viwanda na wanasheria.

Chini ya mpango wa OFAB Media Awards (OMAs), walioshiriki shindano la 2022 walihusisha majukwaa ya magazeti, tovuti za vyombo vya habari, runinga na redio.

Agatha Ngotho, ambaye ni mwandishi gwiji wa masuala ya kilimo aliibuka kidedea akitia kibindoni zawadi ya Sh100,000 pesa taslimu na kombe la shime.

Agatha huripotia Gazeti la The Star linalomiliwa na Radio Africa Group.

Vincent Anguche wa Radio Citizen (Royal Media Services) na Victor Muturi anayeripotia Radio France International, walishikilia nafasi ya pili bora kuteuliwa kwao kwa pamoja kukiwakilisha nafasi ya pili na tatu.

Vincent Anguche (kulia) akikabidhiwa hundi kutoka kwa OFAB. PICHA | SAMMY WAWERU

Wawili hao walituzwa Sh60,000 kila mmoja, na kombe la shime.

Uhalisia Kisayansi na makala, uwazi na kuelewa kwa kina mfumo wa Bioteknolojia kuboresha kilimo ni kati ya vigezo vilivyotumiwa na majaji wa muda kupata washindi.

Majaji aidha walitoka kwenye taasisi za kilimo na vyombo vya habari.

Barani Afrika, nchi 10 hutambua wanahabari wanaohamasisha matumizi ya Bayoteknolojia katika shughuli ya kilimo.

Akizungumza katika hafla kutuza washindi, mwenyekiti OFAB tawi la Kenya Dkt Margaret Karembu alisifia juhudi za vyombo vya habari kueneza kampeni ya bioteknolojia.

Mwenyekiti OFAB tawi la Kenya, Dkt Margaret Karembu, akihutubu jijini Nairobi katika hafla ya kutuza wanahabari. PICHA | SAMMY WAWERU

Alisema mchango wa mashirika ya habari umesaidia kwa kiwango kikubwa kuhamasisha wakulima kuhusu mfumo huo.

“Kuepuka kusambaza ripoti potovu, ninahimiza wanahabari wanaodhamini Sayansi kukagua ukweli na uhalisia kupitia watafiti na wataalamu,” akashauri.

Dkt Karembu pia ni Mkurugenzi Mkuu International Service for Acquisition of Agri-Biotech Applications (ISAAA) Afri Center, na aliahidi kwamba mashirika anayoongoza yataendelea kutambua waandishi wanaohamasisha Bioteknolojia.

Shindano la mwaka huu lilikuwa makala ya sita, Afisa Mkuu Mtendaji, East Africa Grain Council Bw Gerald Masila akielezea kusikitishwa kwake na suala la mashamba mengi nchini kugeuzwa majengo ya kukodi.

Afisa huyo alisema hatua hiyo inahatarisha jitihada kuangazia usalama wa chakula, uhaba na njaa.

“Amerika imetushinda kuzalisha mahindi kwa sababu ya kukumbatia mifumo ya teknolojia za kisasa kwenye kilimo. Inazalisha tani 15 kwenye hekta moja ila Kenya ni tani 4 pekee,” akaelezea.

Bw Musila alitaja Bayoteknoljia kama vumbuzi ambayo ikikumbatiwa nchini itaangazia kero ya njaa.

Ni mfumo unaojumumuisha bunifu za kuongeza jeni, kuboresha mimea na mifugo ili kupata spishi zilizoboreka kusaidia kupambana na kero ya kiangazi, wadudu na magonjwa.

Hali kadhalika, unasaidia kuafikia usalama wa mazao kwa kupunguza matumizi ya kemikali.

Kando na manufaa hayo, unashusha gharama ya uzalishaji wa mazao na chakula.

Siku kadha zilizopita, serikali iliondoa marufuku ya uagizaji kutoka nje ya nchi bidhaa za GMO na mimea iliyoidhinishwa na taasisi husika.

Marufuku hayo yaliwekwa 2012.

  • Tags

You can share this post!

Mashujaa Dei: Rais Ruto awahimiza Wakenya wajitolee...

Wamatangi atoa mwelekeo wa ajenda yake

T L