• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:59 PM
Ulanguzi wa dawa za kulevya ulifanya mzungu kunitema

Ulanguzi wa dawa za kulevya ulifanya mzungu kunitema

NA KALUME KAZUNGU

MUDHAFAR Yusuf Musa ni mwenye majonzi tele kila anapotafakari jinsi miaka 10 ya ulanguzi wa dawa za kulevya aina ya heroni na kokeni ilivyopelekea kumpoteza mchumba wake mzungu.

Bw Mudhafar,31, mzawa wa mtaa wa Langoni, kisiwani Lamu alijitosa kwenye ulanguzi wa heroni na kokeni kisiri mwaka mmoja baada ya kubahatika kupendwa na mwanadada huyo mzungu kutoka nchini Uhispania.

Walipatana kwenye mojawapo ya ufukwe wa Lamu mnamo 2010, wakati huo Bw Mudhafar akiwa miongoni mwa vijana wa kutoa huduma za matembezi ya watalii ufuoni.

Kulingana na Bw Mudhafar, yeye alijitosa kwenye kazi za matembezi ya watalii ufukweni baada ya kuacha masomo yake ya sekondari akiwa kidato cha pili kutokana na ufukara wa kifamilia.

Anasema mamake alikuwa mjane baada ya babake mzazi kufariki yeye akiwa darasa la saba kwenye shule ya Msingi ya wavulana ya Mahmoud Bin Fadhil iliyoko mtaa wa Mkomani kisiwani Lamu.

Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi, alijiunga na shule ya upili ya wavulana ya Lamu Bujra ambayo pia inapatikana kisiwani Lamu.

Bw Mudhafar anasema ilimlazimu kukatiza masomo yake na kujitosa katika kazi za watalii ufuoni akiwa umri wa miaka 18 pekee baada ya karo kushindikana.

Ni wakati akiwa mhudumu wa ufuoni mnamo 2010 ambapo alipatana na mrembo wake Mhispania waliyepanga kwamba wangeendeleza penzi lao hadi kufunga pingu za maisha baadaye.

Aliambia Taifa Leo kuwa mchumba wake alikuwa akimpenda kwa dhati kwani kila mara alikuwa akimsambazia mabunda ya pesa, hali iliyomfanya kuanza kujaribu maisha ya starehe, hasa kuvuta bangi.

Anataja vile yeye na mchumba wake walikuwa wakisafiri sehemu mbalimbali za visiwa vya Lamu kujivinjari tu ilmradi wapenzi hao wagandane mithili ya kupe kwenye mkia wa ng’ombe.

Bw Mudhafar aidha alisema kilichomsukuma yeye kuingilia ulanguzi wa heroni na kokeni ni rafiki yake wa karibu ambaye pia alikuwa akichumbiana na mwanadada mtalii kutoka ng’ambo.

“Rafiki yangu wa karibu ambaye tulikuwa tukifanya kazi za kutembeza watalii ufuoni pia alibahatika kupendwa na mrembo kutoka ng’ambo. Ni katika hali hiyo ambapo alinikaribia na kunirai kwamba nitumie heroni kwani nikifanya hivyo nitafaulu kuongeza ashiki kitandani kwa muda mrefu, hivyo kuepuka kuachwa mataani na mchumba wangu ambaye alikuwa msichana mrembo na mwanataaluma ya udaktari kutoka Uhispania. Kutokana na tamaa niliyokuwa nayo, na kwa sababu sikutaka kuachwa, nikazama mzimamzima kwenye ulanguzi wa heroni, japo kisiri. Sikutaka mchumba wangu ajue nilichotumia,” akasema Bw Mudhafar.

Aliendelea na ulanguzi huo kwa miaka kadhaa, ambapo awali, shughuli za kitandani zilifanyika vyema hadi kufikia kiwango cha mchumbake kumshuku kwamba alikuwa akitumia dawa za kuongeza nguvu za kiume.

“Kila aliponiuliza nilikuwa nikimficha na badala yake kumweleza kuwa ulaji wa samaki, hasa pweza na supu yake ndio ulioleta raha yote. Kila nilipomweleza alikubali japo kwa dukuduku. Nikamhakikishia kwamba kila kitu ni shwari na wala sikuwa nikitumia mihadarati yoyote,” akasema Bw Mudhafar.

Anaeleza kuwa asichokijua ni kwamba kila alipotumia heroni, ndivyo ilizidi kumuingia na kukubali mishipa ya mwili kiasi kwamba ikageuka sasa kuwa uraibu wa kupindukia.

Anasema kwa siku alikuwa akitumia kati ya Sh5000 hadi Sh6000 kununua heroni ili kukimu kiu cha dawa.

Alisema ilifikia wakati ambapo yeye hakutaka lolote kutoka kwa mchumba wake isipokuwa fedha tu za kununua dawa za kulevya.

“Mchumba wangu alianza kunishuku kwamba mimi ni mlanguzi wa dawa za kulevya. Nilikuwa sipendi tena kukaa naye karibu au muda mrefu. Kila aliponitajia kuhusu tendo la ndoa nilijitia hamnazo. Nilitaka tu niwe na yeye karibukaribu na punde aliponipa mkwanja, nilitoa udhuru na kumwacha huku nikichomokea mitaani kujitafutia heroni,” akasema Bw Mudhafar.

Mwishowe mchumba wake alifahamishwa na marafiki wake wa karibu suala la yeye kutumia heroni, hali iliyomvunja moyo pakubwa.

Kati ya mwaka 2018 na 2019, mchumba wake alijaribu kumrai kuacha matumizi ya dawa za kulevya endapo yuko na nia yoyote ya kumuoa siku za usoni.

“Uchumba wetu ulikuwa umekomaa vilivyo kwani tulikuwa tuko karibu mwaka wa nane. Nilikuwa nimemtambulisha kwa wazazi wangu na yeye pia kwa wazazi wake. Lakini baada ya mimi kugeukia uraibu alichoka kunirai niache uraibu. Mwaka 2020, mchumba wangu akaniita na kuweka bayana kwamba ameniacha,” akasema Bw Mudhafar.

Anasema miezi michache baadaye, mchumba huyo mtalii aliabiri ndege na kurudi zake Uhispania. Pia alikatiza kabisa mawasiliano kati yake na Bw Mudhafar.

Anasema baada ya kuachwa na mchumba wake, maisha yalibadilika na kuwa magumu kwani hakuwa na kazi yoyote ilhali muda mwingi akiupoteza katika ulanguzi wa heroni.

Alifichua kuwa kutokana na ughali wa kukimu maisha ya ulanguzi wa heroni na ukosefu wa fedha, aligeukia maisha ya wizi, ambapo alikuwa akimwibia mpaka mamake mzazi ilmradi apate cha kuuza na kununua heroni akate kiu.

“Jamii ilianza kunichukia. Niliuza karibu kila kitu nyumbani kwetu, ikiwemo dhahabu za mamangu. Ndugu na dada zangu walinikasirikia na kuniogopa kutokana na mienendo michafu niliyokuwa nayo. Majirani kila wakiniona walinifurusha kama mbwa wakijua fika niko sehemu yao kuwaibia. Maisha yalikuwa magumu si haba,” akasema Bw Mudhafar.

Anataja maisha ya uraibu wa heroni kuwa sawa na yale ya hayawani kwani mja huwa hajali ubinadamu, uzuri wala ubaya.

“Lawama kwangu zilikuwa ni kama manukato. Sikujali kuwaibia wazee, vijana na akina mama bidhaa zao, ikiwemo simu ilmradi nipate cha kuuza ninunue heroni. Kuna wengine hata niliwadhuru kwa kuwapiga na kuwapora vitu vyao viochochoroni mchana na usiku. Mamangu alikuwa akiletewa kesi na majirani karibu kila siku. Kwa wakati wote, mimi sikuambilika wala kusemezeka kwani nilikuwa mimi na heroni, heroni na mimi,” akasema Bw Mudhafar.

Aidha kufikia mwaka wa 2021 na baada ya maisha ya uraibu kuzidi kumlemea, Bw Mudhafar anasema alianza kutafakari kuhusiana na mustakabali wa maisha yake ya siku za usoni.

Mudhafar Yusuf Musa,31, akiwa na Ustadh Swale Said (kulia). PICHA | KALUME KAZUNGU

Alitafakari jinsi heroni ilivyoharibu asilimia kubwa ya maisha ya ujana wake, akawaza na kuwazua kama kulikuwa na faida yoyote. Akakuta ni hasara tu.

“Hapo ndipo nilipoamua kuupiga teke uraibu japo kwa ugumu tele. Kwa bahati nzuri, ilipofika Machi 5, 2021, kituo cha matibabu ya methadone kilifunguliwa kwenye hospitali kuu ya King Fahd mjini Lamu kupitia Shirika la muungano wa Waislamu-MEWA. Sikupoteza muda bali nilijisajili na kuwa miongoni mwa wateja wa kwanza kwanza kituoni humo. Tangia hapo hadi sasa nimekuwa nikipokea ushauri nasaha na tiba ya methadone ambayo imeniwezesha kabisa  kuacha heroni. Ni mwaka wa tatu sasa bila kulangua heroni au kokeni,” anaeleza Bw Mudhafar.

Anasema wakati wa aushi yake akiwa teja, katu hakupendwa na wanawake kwani alikuwa mchafu na mtu aliyeonekana hatari kukaribiwa.

Mudhafar Yusuf Musa,31, hupenda kupokea mawaidha kutoka kwa viongozi wa kidini Lamu. PICHA | KALUME KAZUNGU

Aidha tangu alipoanza matumizi ya medhadone mkiaka mitatu iliyopita, Bw Mudhafar amekuwa miongoni mwa watu nadhifu ambao wanapendwa na wengi kisiwani Lamu kwani ni kupitia kuacha matumizi ya dawa za kulevya ambapo heshima yake pia ilirejea.

“Baada ya kuacha uraibu wa heroni, niliafikia sasa kuwa mtu wa heshima kwa wote. Hata warembo walianza kunipenda na kunikaribia. Agosti, 2022, nilipendana na mrembo Mswahili wa asili ya Kibajuni kama mimi kwa jina Sumeiya Aboud kutoka kijiji cha Mbwajumwali huko Lamu Mashariki. Tulifunga pingu za maisha mwezi huo na kwa sasa tumebarikiwa mtoto mmoja. Mke wangu pia ni mjamzito wa miezi sita. Kwa sasa mimi ni mwenye furaha tele,” akasema Bw Mudhafar.

Anawashauri vijana kujiepusha na ulanguzi wa dawa za kulevya, akisisitiza kuwa kuingia ni rahisi lakini kutoka ni ngumu.

“Yale nimepitia heri mtu akuroge, akudunge kisu ufe au akuambukize Ukimwi kuliko kukurai kujitosa kwenye lindi la mihadarati. Mihadarati maisha yake ni ya hayawani. Vijana wajali maisha yao. Jiepusheni na marafiki wabaya na kuwa raia wema. Miaka yote 10 ya ujana wangu sijaifurahia kamwe. Tubadilike tuishi.  Nafurahia maisha kikamilifu sasa baada ya kujinasua kutoka kwa heroni,” akasema Bw Mudhafar.

Ujumbe kwa ex wake mzungu ni kwamba bado anamshukuru kwa kutenga muda wake kufurahia maisha na yeye kwa zaidi ya miaka 10.

“Najuta kumpoteza mchumba wangu mzungu na hata sasa ninamuomba msamaha. Nimejaribu hata kumtafuta mtandaoni na kumuongelesha. Mimi nimebadilika kikamilifu sasa. Nimeacha uraibu nina mke. Nafurahia sana. Najua mrembo mzungu nilikuvunja moyo kutokana na tabia zangu potovu wakati huo. Niwie radhi,” anasema Bw Mudhafar.

  • Tags

You can share this post!

Gavana awakashifu wanaokosoa rekodi yake ya maendeleo

Hii ni kwa wanaonyonyesha na inawabidi kuenda kazini

T L