• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Profesa Oduor: Mifumo ya Bioteknolojia hupitia kaguzi za kina za Kisayansi kabla kuidhinishwa

Profesa Oduor: Mifumo ya Bioteknolojia hupitia kaguzi za kina za Kisayansi kabla kuidhinishwa

NA SAMMY WAWERU

MWANASAYANSI na Mtafiti kutoka Chuo Kikuu cha Kenyatta (KU) amewataka wakulima kupuuzilia mbali madai ya wakosoaji wa mifumo ya Bayoteknolojia katika kuzalisha chakula.

Prof Oduor ambaye ni Mhadhiri wa Kitengo cha Biolojia ya Molekuli, amesema habari zinazoenezwa na wanaopinga Bayoteknolojia ni potovu na zisizo na msingi wowote Kisayansi.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, mtafiti huyo amesema uhaba wa chakula unaokumba Bara Afrika utaangaziwa endapo sekta ya kilimo itakumbatia mifumo na bunifu kufanya kilimo endelevu.

Baadhi ya wanaharakati wamekuwa wakitilia shaka mifumo ya Bioteknolojia, hasa ukuzaji wa mimea iliyoboreshwa jeni (GMO).

“Tuipe nafasi mifumo ya bioteknolojia, inaweza ikatatua changamoto za uhaba wa chakula,” Prof Oduor akasema.

Mtaalamu huyo mwenye msingi wa Uhandisi wa Jeni, Utafiti wa Dawa na Uchunguzi wa Masuala ya Kisayansi alisema kuafikia mifumo endelevu ya chakula Afrika haina budi ila kutathmini mikondo yake kuangazia uzalishaji.

Mwanasayansi katika Chuo Kikuu cha Kenyatta Prof Richard Oduor. PICHA | SAMMY WAWERU

Upembe wa Afrika, unaojumuish Kenya, Somalia na Ethiopia umeathirika pakubwa kutokana na janga la ukame.

Mabadiliko ya tabianchi yanazidi kuonyesha makali, licha ya Afrika kukadiriwa kuchangia asilimia 4 pekee ya gesi hatari ambazo zinaharibu mazingira.

Kukwepa athari hizo, wakulima wanahimizwa kukumbatia mifumo ya bioteknolojia na mimea iliyoboreshwa kiasi cha kuhimili kiangazi, ukame, wadudu na magonjwa.

Prof Oduor anasema kabla ya mifumo na bidhaa za GMO kuidhinishwa, huwa zimepitia utafiti na uchunguzi wa kina Kisayansi.

“Hupitia tafiti za kina na majaribio kwenye maabara,” akasisitiza.

Mdahalo wa GMO hata hivyo umezua hisia tofauti, hasa miongoni mwa viongozi na wanasiasa.

Mwezi Novemba, Mahakama Kuu ilisimamisha kwa muada uagizaji chakula cha GMO kutoka nje hadi pale kesi iliyowasilishwa itakapoamuliwa.

Rais William Ruto aliondoa amri ya uagizaji bidhaa hizo iliyowekwa mwaka wa 2012.

“Tuna uwezo na vifaa vya kutosha kupiga msasa mifumo ya bioteknolojia na bidhaa zake.

“Isitoshe, ukaguzi ni zoezi la muda mfupi kwenye maabara,” Prof Oduor akaelezea.

Kupitia Sheria ya Bunge 2019, Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama wa Bidhaa ilizinduliwa.

“Chini ya muda wa miaka 10 ambayo bidhaa za GMO zilikuwa zimepigwa marufuku, visa vya Saratani vimekuwa vikiripotiwa. Kwa nini bidhaa zilizoboreshwa jeni zinakosolewa ilhali tuna mamlaka kubaini usalama wake?” akataka kujua mhadhiri huyo.

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Saladi ya kuku, maembe na tango

Kongamano kujadili mifumo ya afya barani laanza

T L