• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:03 PM
RIZIKI: Mtangazaji wa redio asiyechagua kazi

RIZIKI: Mtangazaji wa redio asiyechagua kazi

Na SAMMY WAWERU

KIJANA John Ngugi ni ‘Jack wa biashara zote’, ambapo mbali na kuwa mtangazaji wa redio, hufanya biashara za hapa na pale.

Huburudisha mashabiki katika kituo cha redio cha Hood – ambacho hupeperusha matangazo yake kupitia mitandao. Ngugi ni barobaro mwenye bidii za mchwa, akifichua kwamba wakati hayupo hewani kuburudisha mashabiki wake, huwa jikoni.

“Mimi ni mpishi wa chapati, na hutafuta vibarua kwenye mikahawa kupika chapati,” anaelezea kijana huyo. Ana ufasaha wa Kiswahili ambapo huburudisha wasikilizaji wake kwa lugha hii teule.

Hata ingawa kwenye redio hujitolea kufanya kazi bila malipo, anasema hujiendeleza kimaisha kwa kufanya vibarua vya mapishi katika mikahawa.

Isitoshe, ni mfanyabiashara wa misimu, kauli ‘Mchagua jembe si mkulima’ ikimuongoza. Ngugi si mchaguzi wa kazi na Sikukuu ya Valentino 2021 alikuwa kazini.

Februari 14, ilikuwa siku yenye shughuli chungu nzima kwa kijana Ngugi. Ikiwa siku ya Valentino na iliyolingana na Jumapili, Ngugi alijituma kuzimbua riziki.

Aidha, tulimpata katika lango la Kanisa la Deliverance, Zimmerman, kiungani mwa jiji la Nairobi, ambalo pia lina Shule ya Kibinafsi ya Cornerstone Academy, ambapo alijituma kuhudumia waumini na wapita njia.

Akiwa amevalia nadhifu, aliandaa meza iliyositiri mashada ya maua maridadi yaliyogharimu kati ya Sh500 – 2, 000.

Kwenye mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali, alifichua kwamba alikita kambi eneo hilo saa mbili asubuhi.

“Ninaamini bidii huondoa kudura. Hata ingawa sijawahi kuuza maua siku ya Valentino, ninayaridhia, inaonekana ni biashara yenye mapato hata ikiwa ni ya muda,” akasema.

Alisema kati ya saa tatu na saa nne, alikuwa amefanya mauzo ya mashada yasiyopungua matano, huku kati ya saa nne na saa tano akiwa ameuza zaidi ya 10.

“Siku inapozidi kukucha, ndipo mauzo yanaendelea kuongezeka. Kati ya saa tano hadi saa sita, niliuza zaidi ya mashada 15,” Ngugi alidokeza.

Alisema chaguo kukita kambi nje ya kanisa, lilichochewa na mila na tamaduni za idadi kubwa ya Wakenya ambao siku ya Jumapili hukongamana maeneo ya kusali na kuabudu.

“Kanisani wahubiri hutufunza kuhusu upendo. Siku ya leo (Februari 14, 2021) ni mojawapo kuonyesha mapenzi zaidi kwa jamaa, wanandoa na pia wachumba. Nimeona wazazi wakinunulia watoto wao chokoleti na pia maua, kabla na baada ya kuingia kanisani,” alifafanua mtangazaji-mfanyabiashara huyo.

Kila shada alilouza liliandamana na chokoleti na peremende zenye nembo ya upendo. Valentino ni siku maalum ya wapendanao inayoadhimishwa Februari 14 kila mwaka.

Mbali na wapendanao, siku ya Valentino pia kuna watoto wanaoitumia kuonyesha upendo wao kwa wazazi, na wazazi kwa watoto.

Vilevile, wengine huonyesha mapenzi kwa kutembelea vituo vya watoto yatima na walioachwa.

Ni katika jukwaa la siku hiyo, ambapo Ngugi alifichua kwamba yeye ni mtangazaji katika kituo cha redio cha Hood, ambacho hupeperusha matangazo yake kupitia mitandao.

“Ninaienzi lugha ya Swahili, na ndio maana hupeperusha vipindi kwa lugha hii teule kuongoa na kuburudisha mashabiki wangu,” alielezea.

Barobaro huyo anahimiza vijana kutochagua kazi, muradi ni halali ili waweze kujiendeleza kimaisha badala ya kusubiri na kutegemea ajira za ofisi na ambazo ni finyu nchini.

You can share this post!

Chanjo ya corona kutua Nairobi Jumanne

Kampuni za humu nchini haziruhusiwi kuagiza chanjo –...