• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Wawaniaji walilia IEBC wakidai serikali ya Joho inawanyanyasa

Wawaniaji walilia IEBC wakidai serikali ya Joho inawanyanyasa

NA WINNIE ATIENO

WANASIASA wapinzani wa chama cha UDA katika Kaunti ya Mombasa, sasa wanaitaka Tume ya Uchaguzi (IEBC), iingilie kati wakizidi kulalamikia unyanyasaji kutoka kwa serikali ya kaunti.

Wanasiasa hao wanaogombea viti mbalimbali vya kisiasa wamedai kuwa licha ya malalamishi yao ya awali, serikali ya kaunti hiyo inayoongozwa na Gavana Hassan Joho, inaendelea kuwanyima nafasi ya kuweka mabango yao na kutumia viwanja wanavyohitaji kwa mikutano ya hadhara kabla ya uchaguzi wa Agosti 9 kufika.

Serikali ya kaunti hiyo ilikuwa imepinga madai hayo, ikisema malalamishi hayo hayana msingi na yametokana na uoga wa wanasiasa wenyewe katika ushindani wa kisiasa.

“Tunataka usawa katika kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuuu. IEBC iingilie suala hili maanake kuna ubaguzi,” alisema mgombea wa ugavana Mombasa kupitia chama cha Vibrant Democratic Party (VDP), Bw Hezron Awiti Bollo.

Mwenzake ambaye anawania useneta, Bw Cornelius Mutune (UPIA) na mgombea huru wa ubunge wa Nyali, Bw Eric Gitonga, walisema mienendo ya kaunti hiyo si haki kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu.

Baadhi yao walitishia kuweka mabango kwa lazima iwapo wataendelea kunyanyaswa, huku Bw Gitonga akisema watauza sera kwa kubandika makaratasi.

Hivi majuzi, mwaniaji wa ugavana kupitia Chama cha UDA, Bw Hassan Omar, alimshtumu Bw Joho kwa kumnyima nafasi ya kuegesha mabango yake mitaani.

Bw Joho ndiye naibu kiongozi wa Chama cha ODM, ambacho kimemsimamisha Mbunge wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, kama mgombeaji wake wa ugavana katika uchaguzi unaosubiriwa.

  • Tags

You can share this post!

Serikali kutoa dawa za minyoo kwa watoto milioni 6

Presha katika ODM kuzuia wafuasi kususia uchaguzi

T L