• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Shakahola: Wanaotafuta jamaa wasema ngoja ngoja yaumiza

Shakahola: Wanaotafuta jamaa wasema ngoja ngoja yaumiza

ALEX KALAMA Na FARHIYA HUSSEIN 

ZAIDI ya familia 93 za waliopigiwa simu kuenda kuchukuliwa sampuli za vinasaba (DNA) zina matumaini ya kwamba wataunganishwa na wapendwa wao.

Lakini licha ya kuchukuliwa vipimo hivyo hadi sasa wengi hawajaweza kupata wapendwa wao huku matumaini ya kuwapata wakiwa hai yakizidi kudidimia.

Ruth Kadzo Kahindi kutoka kijijii cha Kanagoni kilichoko wadi ya Adu katika eneobunge la Magarini ni miongoni mwa watu kutoka familia hizo zinazotafuta jamaa zao waliopotea.

Bw David Kahindi akiwa na mke wake Ruth Kadzo Kahindi katika eneo la Kanagoni kwenye Kaunti ya Kilifi mnamo Mei 10, 2023. Wanatafuta jamaa zao tisa ambao inadaiwa walikuwa wafuasi wa mafundisho ya mhubiri Paul Mackenzie ambaye ni mshukiwa wa maafa yaliotokea msituni Shakahola. PICHA | KEVIN ODIT

Kufikia sasa hajui waliko jamaa zake tisa, hii ikiwa ni pamoja na mwanawe Mary Smart, wajukuu wake sita na vitukuu wawili wanaoaminika walikuwa waumini wa dhehebu tata la Good News International.

“Nilipigiwa simu nikapeleke sampuli zangu za DNA lakini hadi sasa majibu sijapata. Niko gizani na sijui ni nini cha kufanya. Pia, hatujaruhusiwa pia kuangalia ile miili ili kutambua watu wetu ikiwa walifariki,” alisema Bi Kahindi.

Kulingana naye Bi Kahindi mkwe wake aliyekamatwa Bw Smart Mwakala ambaye inadaiwa ni msadizi wa karibu wa mhubiri tata Paul Mackenzie amekataa kusema waliko wanafamilia hao.

“Mume wa mjukuu wangu wa kwanza ndiye aliyeokolewa peke yake, na alidai kwamba vitukuu wangu wawili ndio waliokuwa wa kwanza kuzikwa baada ya kufa njaa,” alisema Bi Kahindi.

Bi Kahindi alieleza zaidi kuwa safari yake haikuwa kazi rahisi kwani alilazimika kusafari umbali wa kilomita 55 kila mara hadi mji wa Malindi ili kuchukuliwa sampuli za DNA na pia kutoa taarifa kwa maafisa wa upelelezi Malindi kuhusu yale ambayo anayafahamu.

Vilevile raia wa Nigeria Bw Abbas Babatunde anayetafuta mke wake na mwanawe alisema ameshapeleka sampuli zake kwa ajili ya uchunguzi.

Raia wa Nigeria Bw Abbas Babatunde anayetafuta mke wake na mwanawe. PICHA | ALEX KALAMA

“Ndio, nishatolewa sampuli ila bado sijui waliko watu wangu. Inasikitisha kuwa hatuwezi kuona miili ya wale waliofukuliwa. Tunaambiwa tusubiri majibu,” alisema Bw Babatunde.

Anatafuta, mke wake, mwanawe, baba mkwe, mama mkwe, na mashemeji wake wawili.

Kwa sasa, picha waliopiga pamoja ndiyo inasalia kumkumbusha fursa na wakati wa kufana siku za nyuma huku akiwa na wasiwasi ikiwa atawaona tena.

Bw Rodgers Mwibo aliyekosa nauli na malazi alilazimika kupeleka sampuli zake katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) jijini Nairobi.

“Kabla ya safari yangu kurudi Nairobi, nilihoji watu kadhaa walioniarifu dadangu na binamu yangu walikufa na kuzikwa Shakahola, ila sikuhurusiwa kuenda kuangalia makaburi yao. Mamangu aliyekuwa na wao naelezewa alibadili jina lake Pamela na sasa anajulikana kama Rose,” akasema Bw Mwibo.

  • Tags

You can share this post!

Kufikia jana Jumatano idadi ya walioangamia Shakahola...

Inter Milan wapepeta AC Milan na kutia guu moja ndani ya...

T L