• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
TAHARIRI: Kampeni ghali ndizo zinazotuchongea

TAHARIRI: Kampeni ghali ndizo zinazotuchongea

KITENGO CHA UHARIRI

RIPOTI iliyotokana na utafiti mmoja hivi majuzi imeonyesha uhalisia wa jinsi uchaguzi nchini ulivyo ghali.

Na katika muktadha huo huo, kuonyesha kwa nini kama taifa tutaishia kulia kuhusu uporaji wa mali ya umma na mwendo wa kinyonga wa maendeleo hasa yale tunayotarajia kutoka kwa wanasiasa tunaochagua.

Ripoti hiyo iliyoitwa ‘The cost of politics in Kenya: Implications for political participation and development’ ya Karuti Kanyinga na Tom Mboya iliyochapishwa Julai imethibitisha kwamba pesa ndio zinazonunua hatamu za uongozi.

Kwamba wanasiasa wanaotumia pesa nyingi zaidi ndio wanaochaguliwa huku wale wa mifuko midogo, licha ya sifa nzuri za uongozi wanaishia kukaa nje kwenye kibaridi.

Aidha, imeonyesha pia kuna maeneo ya humu nchini ambayo ni ghali zaidi kutafuta nafasi ya uongozi huku viti vya useneta vikiwa ndio ghali zaidi kupigania.

Kwa kadri, mwaniaji wa viti vya kaunti anahitaji takriban Sh45 milioni za kampeni huku maeneo ya Nairobi, Nyanza na Magharibi yakionekana kuwa ghali zaidi.

Seneta mmoja ananukuliwa na ripoti hiyo akisema kwamba alitumia hadi Sh100 milioni kupigania kiti hicho.

Suala la kampeni kote duniani huwa linahusu pesa nyingi, lakini tofauti na hapa kwetu na mataifa kama Amerika, ni kwamba wafuasi wa mwanasiasa ndio huchanga pesa kufadhili kampeni hizo.

Hii husaidia umma kuwa washiriki kamili wa mchakato mzima wa uchaguzi na demokrasia kwa sababu ni pesa zao zinatumika; hivyo basi kuwapa shime ya kuchagua mwanasiasa aliye bora zaidi kwenye mchujo.

Lakini ukilinganisha na hapa nchini, wapigakura hawachangii kampeni, bali wanasubiri kushawishiwa na wanasiasa na ushawishi huu ukiwa kwa mfumo wa pesa.

Na hapa ndipo unajiuliza, mwaniaji huyo anatoa wapi kitita cha hadi Sh100 kupigania kiti hicho? Na akikipata, atatumia muda wake kufanya nini haswa kama sio kujilipa mamilioni hayo na kutafuta zingine za uchaguzi ujao.

IEBC ilikuwa imeleta matumaini ilipotangaza kwamba inaunda sera za kudhibiti pesa katika kampeni lakini hata kabla kubadili nia na kutupilia mbali mapendekezo ya kanuni hizo, tayari ilikuwa ishaanza kupondwa kwa kiasi kikubwa cha pesa ambacho tayari ilikuwa imependekeza.

Ikiwa tunataka kampeni za ukweli na za watu wanaostahiki, itabidi tuwazie hili suala la fedha katika kampeni.

You can share this post!

Arudi na zawadi alipokosa mlo harusini

Pendekezo la mchujo wa ODM laibua hofu

T L