• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
UJASIRIAMALI: Watumia teknolojia kupata wateja wa mboga na matunda salama kwa afya

UJASIRIAMALI: Watumia teknolojia kupata wateja wa mboga na matunda salama kwa afya

NA MARGARET MAINA

URAFIKI wa Seif Waziri, 25, na Paul Rugendo, 23, ulianza mwaka wa 2017 wakiwa chuoni na umekua hadi wakaanza kufanya ushirikiano wa kibiashara.

Wawili hao ni waanzilishi wa Siha Organic Grocery Stores, duka la rejareja la mtandaoni ambalo huuzia wateja chakula cha bei nafuu na chenye tija kwa afya.

Kuingia kwenye biashara ilikuwa rahisi. Walipokuwa wakiendeleza elimu yao ya digrii katika Chuo Kikuu cha Egerton, waligundua kuwa kulikuwa na uwezekano wa biashara kwa mazao mjini Nakuru. Kulikuwa na wafanyabiashara wachache ambao wangeweza kuthibitisha kwa kuridhisha ili kutoa hakikisho kuhusu usalama wa chakula kwa wateja.

Ilisaidia pia kwamba Paul alikuwa na shauku ya kilimo na Seif alikuwa mpenda mazoezi ya mwili. Kuanzisha biashara inayojumuisha kilimo na lishe, kwa hivyo ilikua lengo lao. Na kwa hivyo mnamo 2020, walianzisha biashara hiyo.

Wakiwa na mtaji wa Sh1 milioni, walitafuta shamba huko Nyeri, kufungua wavuti wa biashara kupata wateja wa mtandaoni na kufungua duka.

“Tumejitolea pia kutoa ushauri maalum wa lishe kwa watumiaji wetu kutoka kwa mama wajawazito na wanaonyonyesha hadi watu wanaopambana na magonjwa ya mtindo wa maisha,” anasema Paul.

Japo vyakula salama huchukuliwa kuwa ghali, Siha Organics imeanzisha gharama ya chini ya uzalishaji, gharama ya chini ya usambazaji na mbinu ya soko kubwa ili kusaidia kudumisha bei ya kiwango cha chini.

Wateja wakuu wa Siha Organics ni kaya za kipato cha kati ambao hufikia bidhaa zao kwa kuagiza mtandaoni kwenye tovuti yao au kupitia simu. Pia wanatoa huduma zao kwenye mikahawa na vibanda.

“Tuna vifurushi vinne vya thamani ambavyo vinajumuisha matunda na mboga tofauti. Vifurushi hivyo bei yake ni kuanzia Sh500 hadi Sh2,000. Wateja huweka agizo lao kupitia tovuti yetu, huendelea kulipa na kuingiza maelezo ya bili na maagizo yao yanawasilishwa mlangoni mwao kwa ada.”

Biashara imekuwa nzuri, kiasi kwamba wanapata Sh25,000 kwa wastani wa faida ya kila mwezi.Wana wafanyikazi watatu wa kudumu na vibarua watano wa kawaida wa shambani.

Bidhaa ndani ya duka la Siha Organic Grocery Stores lililoanzishwa na Seif Waziri, 25, na Paul Rugendo, 23. PICHA | MARGARET MAINA

Wateja wao wana aina nyingi za matunda na mboga karibu 35 ambazo wanaweza kupata kutoka kwa duka.

Wawili hao wanaashiria kuanzisha maduka zaidi katika jiji la Nakuru na kote nchini. Pia wanalenga kuongeza uwezo wao wa uzalishaji.

“Gharama ya jumla ya chakula imekuwa ikiongezeka. Kaya nyingi haziwezi kumudu kula chakula bora. Tunalenga kutatua tatizo hili na tayari bei zetu ndizo zinazoshindana zaidi sokoni.”

Kupata mazao kwa bei nafuu na kuthibitishwa kutoka kwa wakulima wadogo imekuwa miongoni mwa changamoto zao kuu.

“Usafirishaji wa mazao kutoka mashambani hadi dukani pia umeonekana kuwa changamoto kubwa, hivyo kuongeza gharama za uendeshaji wa biashara hii yetu,” anasema Paul.

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Kimanda cha viazi mbatata

LISHE: Fahamu faida za kula nyanya mbichi zilizoiva vizuri

T L