• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
VYAMA: Chama cha Kiswahili cha Triple ‘S’ katika shule ya upili Satima, Nyandarua

VYAMA: Chama cha Kiswahili cha Triple ‘S’ katika shule ya upili Satima, Nyandarua

Na CHRIS ADUNGO

CHAMA cha Kiswahili cha Triple ‘S’ ni chombo kinachotumiwa na wanafunzi wa Shule ya Upili ya Satima katika Kaunti ya Nyandarua kuboresha matokeo ya KCSE Kiswahili.

Chama hiki ambacho kimeinua ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi, kiliasisiwa na mwalimu Mwai wa Nguyo kwa kushirikiana na Bw R.M. Kariuki (Naibu Mwalimu Mkuu) mnamo 2018.

Ingawa wakati huo Triple S ilikuwa na wanachama 15 pekee, idadi hiyo iliongezeka zaidi ya maradufu kwa kipindi kifupi na chama kwa sasa kinajivunia wanachama 60.

Mbali na kuweka wazi umuhimu wa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi, madhumuni mengine makuu ya Triple S ni kustawisha matumizi ya lugha shuleni, kupiga jeki shughuli za Idara ya Kiswahili na kupanua mawanda ya utafiti katika nyanja za kitaaluma zinazofungamana na Kiswahili.

Wanachama hukutana kila Jumanne na Alhamisi kuteua maripota ambao hukusanya habari za matukio muhimu yaliyofanyika shuleni kisha kutangaza gwarideni siku za Jumatatu na Ijumaa.

Mikakati hii imewaamshia wanafunzi hamu ya kujitosa katika ulingo wa uanahabari kwa matarajio ya kuwa maripota, wahariri na watangazaji shupavu katika siku za halafu.

Aidha, viwango vya ulumbi, utunzi wa mashairi na kazi nyinginezo bunilizi vimeimarika pakubwa miongoni mwa wanachama ambao shughuli zao zinaungwa mkono kikamilifu na Mwalimu Mkuu, Bw Njoroge Kiarii.

Kubwa zaidi katika mipango ya baadaye ya Triple S ni kubuni kitengo cha maigizo kitakachowapa wanafunzi jukwaa maridhawa la kuigiza vitabu teule vinavyotahiniwa katika Fasihi Andishi na kushiriki tamasha za kitaifa za muziki na drama.

  • Tags

You can share this post!

Rais Kenyatta atia saini mswada tata wa vyama vya kisiasa

Kendia FC ya Ruiru yapiga hatua

T L