• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
WANDERI KAMAU: Tumekisaliti kizazi cha sasa kwa jina la elimu

WANDERI KAMAU: Tumekisaliti kizazi cha sasa kwa jina la elimu

Na WANDERI KAMAU

TANGU jadi, jamii imekuwa ikiichukulia elimu kuwa “ufunguo wa maisha”.Naam, elimu ni njia pekee ya hakika ya kuikomboa jamii kutokana na uchochole, mapuuza na kutojua.

Hadi sasa, elimu huonekana kama njia pekee ya kuwaunganisha na kuwaweka watu maskini na matajiri katika jukwaa sawa.

Pindi watoto wachanga wanapojiunga na shule za msingi, huwa wanapewa mashauri ya kila aina kuhusu umuhimu wa elimu katika maisha yao ya baadaye.

Bila shaka, elimu ni kiunganishi cha watu wa jamii tofauti, tabaka, rangi na dini.Hata hivyo, thamani na umuhimu wa elimu unaonekana kutokuwa kama unavyochukuliwa na jamii.

Kadri siku zinavyosonga, thamani ya elimu inaendelea kushuka kutokana na maovu na changamoto nyingi zinazoiandama.

Vijijini mwetu, watu waliosoma walionekana kama “miungu wadogo”.Waliheshimika na kuthaminiwa pakubwa.

Waliitwa kwenye mikutano katika shule mbalimbali vijijini kuwapa ushauri wanafunzi kuhusu umuhimu wa kutia bidii masomoni.Walionekana kuwa wenye ujuzi na suluhisho kwa kila tatizo lililotokea katika jamii.

“Someni muwe kama Mwafulani!” ingesemwa.“Someni mfike katika vyuo vikuu!” Ndizo kauli ambazo wazazi waliwapa na kuwaelekeza wanao kila mara walipoona wakizembea katika masomo ama kufeli mitihani yao.

Ikizingatiwa kuwa hizi ni kauli ambazo zimepitishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine, elimu katika jamii za Kiafrika imekuwa ikichukuliwa kama “njia ya kuwakomboa wanajamii.”

Kinyume na ilivyokuwa awali, elimu sasa inaonekana kuwa chemchemi ya matatizo yanayoikumba jamii.Ni katika sekta hiyo muhimu ambapo walimu wakuu wa shule za upili wanawanyima nafasi wanafunzi werevu kwa “kuuza” nafasi zao kwa watu matajiri.

Ni katika sekta hiyo ambapo wahadhiri wameripotiwa kushiriki ngono na wanafunzi wa kike ili kuwapa alama za juu kwenye mitihani yao katika vyuo vikuu.

Kana kwamba hayo hayatoshi, ni katika sekta hiyo pia ambapo watu laghai wamekuwa wakighushi vyeti vya shahada ili kupata kazi katika idara za serikali na kibinafsi.

Kupitia maovu hayo, ndoto za wanafunzi werevu kutoka jamii maskini huwa zinasambaratishwa na kuvurugwa na watu wabinafsi na wasiojali hata kidogo.

Ni kupitia maovu hayo ambapo tumekuwa tukisikia visa kuhusu wanafunzi wanaotembea katika shule za upili bila karo na kuwaomba wahisani kujitokeza kuwasaidia.

Mara nyingi, wanafunzi hao hukumbana na masaibu hayo kutokana na mapendeleo ambayo huwepo kwenye taratibu za upeanaji wa basari, hasa katika maeneobunge.

Wale ambao huwa hawabahatiki kupata wahisani hulazimika kuegemea shughuli nyingine ili kujiendeleza kimaisha.

Wengi hukata tamaa kwa kuona ndoto zao za kuwa watu wenye thamani kuu katika jamii kama madaktari zikipotea hivyo tu.Kinaya ni kuwa, wao husalitiwa na jamii ile ile iliyowarai kutia bidii walipokuwa wakianza masomo yao.

Huu ni usaliti wa wazi.Ili kulainisha hali na kurejesha hadhi iliyokuwepo awali kuhusu elimu, ni wakati Waziri wa Elimu, Prof George Magoha, na wakuu wahusika kuzinduka na kumkabili vikali yeyote atakayepatikana akihusika katika uovu wa aina yoyote ile.

Lazima jamii iungane kuleta uwazi uliokuwepo awali katika sekta hiyo muhimu.

[email protected]

You can share this post!

Madiwani Kisumu walaumiwa kwa ziara ya Tanzania

Ruto ainua mikono