• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 12:05 PM
ZARAA: Asema kilimo kinalipa bora hatua zinazofaa zizingatiwe

ZARAA: Asema kilimo kinalipa bora hatua zinazofaa zizingatiwe

NA WYCLIFFE NYABERI

UTAALAMU wa kuotesha uyoga umeanza kushika kasi humu nchini baada ya watu kutilia maanani umuhimu wa lishe bora.

Lakini hadi sasa, ni wananchi wachache tu, wanaofahamu kilimo hicho, licha ya kuwa na manufaa chungu nzima.

Ili kukupa mwangaza jinsi biashara hii inaweza kukunufaisha kwa kukuzolea mapato tele, ukumbi wetu wa Akilimali ulimtembelea mkulima Yabesh Chweya,70, kijijini kwake Amaiga-Bobaracho, eneobunge la Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii kupambanua hali halisi.

Mzee huyu mchungaji wa kanisa la Kiadventista, amekubuhu katika uoteshaji uyoga baada ya kuzama nyanjani miaka 10 iliyopita.

Yeye ni mwanazaraa kitaaluma na amewahi kuishi nchini Marekani kabla ya kurudi Kenya kuanzisha kilimo asichojutia.

“Uyoga upo wa aina mbali mbali na ustawishaji wake hutofautiana kulingana na mahitaji yake. Hii ni pamoja na hali ya hewa, malighafi ya kutosha, urahisi wa teknolojia ya kuotesha katika mazingira tofauti na soko lake,” Mzee Chweya anaanza kutusimulia.

Uyoga anaootesha ni ule unaotumika moja kwa moja kama chakula maarufu kama Oyster au mamama.

Kuna aina nyingine ya uyoga kama ile ya vifundo yaani button mushrooms lakini kwa mzee, mamama ndiyo anayoonea fahari.

Kwa wanaoshikilia dhana kwamba uyoga ni sumu, mzee Chweya anafahamisha kwamba ni chakula bora hata zaidi ya nyama inayoaminiwa na wengi.

Aliamua kugeuza chumba alichokuwa akifugia kuku kukuza uyoga.

Ufugaji wa kuku ulimvunja moyo pale bei ya vyakula ilianza kuwa ghali.

Chumba hicho, amekigawanya sehemu tatu: Kichumba cha kwanza kina malighafi ya maganda ya miwa iliyosagwa maarufu kama bagasse.

Malighafi haya yanapochanganywa na virutubishi vingine, ndiyo hutumika kama mchanga wa kukuza uyoga.

Yeye hupata malighafi hayo kutoka kiwanda cha usindikaji miwa cha Transmara kilichoko Kilgoris.

Kichumba cha pili, ndicho kilichofanyiwa ukuzi wa uyoga na cha mwisho, kina mbegu si haba za uyoga alizozihifadhi kwenye chupa za glasi.

Yeyote anayetaka mbegu hizo, anaweza kuzinunua kwa Sh500 kwa kila chupa.Wakati wa kuotesha uyoga, Mzee Chweya anasema kuna hatua muhimu za kufuatwa.

Hatua ya kwanza ni kuchanganya virutubishi. Malighafi ya bagasse huchanganywa na chokaa ili kuunda mchanganyiko maalum.

Mchanganyiko huo huloweshwa maji na kugeuzwa geuzwa hadi ushikane. Kwa kuwa uyoga humea katika mazingira safi, ni vyema kupitisha malighafi katika mvuke unaotokana na maji yanayotokota kwenye tanuri.

Baada ya hapo, mkulima huyu anasema sasa mchanganyiko unaweza kuwekwa katika karatasi za nailoni, ndoo au magunia yaliyotobolewa mashimo na mbegu kupandwa.

Zao la uyoga hufanya vizuri ndani ya chumba chenye giza almuradi kuwe na mzunguko wa hewa safi.

Kwa muda wa mwezi mmoja, nyunyiza maji kidogo kidogo mchana na jioni kila siku ili unyevu uweze kupunguza kiwango cha joto ndani ya chumba cha ukuzi.

“Mchanganyiko huo utaanza kupata joto ambalo husaidia kuangamiza vidudu hatari, ambao wanaweza kusababisha mkurupuko wa maradhi ambayo ni hatari kwa uyoga,” anaeleza.

Hatimaye kiwango cha joto huteremshwa hadi nyuzi 20 hivi kisha dirisha na milango hufunguliwa ili hewa safi na mwangaza upate kupenya ndani na kufikia uyoga.

Mabadiliko ya ghafla baada ya kuruhusu mwangaza na hewa safi, ndio hufanya uyoga ukaanza kuota na baina ya mwezi mmoja na nusu, uyoga utakuwa umekua kunawiri.

Mkulima anaweza kuendelea kupata mavuno yake kwa miezi minne mtawalia bila kukatika.

Ili kuhakikisha haendi kununua mbegu za uyoga tena kutoka dukani, mzee Chweya hujitengenezea mbegu zake mwenyewe kutoka kwa tishu za uyoga uliovunwa.

Akishatoa tishu hizo, yeye huzichanganya na mtama na kuzihifadhi katika chupa.

Kwa sasa anamiliki mifuko 50 na anasema isingalikuwa ugonjwa wa corona ulioathiri soko la uuzaji bidhaa na kufanya apunguze kiwango chake cha uzalishaji, asingalikuwa katika kiwango alicho.

Hata hivyo, anasema ni muda tu kabla ainuke tena. Katika mzunguko mmoja, mifuko hiyo inaweza kumtolea kilo 500 za uyoga.

Kwa kuwa kilo moja anaiuza kwa Sh 600, hii ina maana ndani ya miezi minne au mitano ya uvunaji, anaweza kuunda Sh 300,000. Unapovuna uyoga, mzee anasema vuna kutumia mikono safi.

“Shika katikati ya shina la uyoga, kisha zungusha hadi ung’oke. Hakikisha umeng’oa kila kitu katika mfuko huo kwani kubakisha shina kunazuia uyoga mwingine kuota,” anaeleza.

Pia anashauri kabla hujavuna, tambua jinsi soko lilivyo ili kuepuka gharama za uhifadhi.

Kwake, huvuna uyoga kulingana na mahitaji ya wateja na anasema kamwe hajawahi kosa wateja wanaotaka bidhaa hii adimu.

Geoffrey Nyakundi, mtaalamu wa lishe katika hospitali moja mjini Kisii, anasema ulaji wa uyoga husaidia kupunguza msukumo wa damu kwa kupunguza viwango vya sukari mwilini.

Pia husaidia mwili kuepuka mzio na vilevile kuwa na kingabora dhidi ya magonjwa mengi.

Lakini cha kumshangaza Mzee Chweya, hakuna kijana hata mmoja aliyewahi kukanyaga nyumbani kwake kumuuliza jinsi anavyoweza kufanya kilimo hicho.

“Vijana wasema hakuna kazi na sioni ikiwa kazi hizo zitapatikana hivi karibuni. Kama vijana wanataka wasaidike, basi hii ndio kazi itakayowakwamua. Kuna hela mchangani ikiwa tu watakubali kuchafuka mikono,” ashauri.

Kwa serikali inayokuja baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti, mkulima huyo anaiomba iimarishe hali ya uchumi wa Kenya ili wakulima wapate masoko ya kuuza bidhaa zao.

  • Tags

You can share this post!

Team Kenya yaapa kuandika historia michezo ya Jumuiya ya...

MITAMBO: Kifaa kinachosaidia kuboresha rutuba

T L