• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
BENSON MATHEKA: Ni makosa maafisa kama Amoth kuhudumu kama kaimu kwa muda mrefu

BENSON MATHEKA: Ni makosa maafisa kama Amoth kuhudumu kama kaimu kwa muda mrefu

NA BENSON MATHEKA

KILA mtumishi wa umma huwa na ndoto moja ya kupanda cheo sekta anayohudumu na serikali imeweka viwango vya kutimiza kabla ya wafanyakazi wake kupandishwa hadhi.

Mojawapo ya mahitaji ya kupandishwa ngazi katika utumishi wa umma ni kuwa na elimu inayotakiwa, kutimiza viwango vya juu vya uadilifu na kuwa na bidii kazini ikiwa ni pamoja na kuonyesha uzalendo kwa nchi yako.

Ikiwa hivi ndivyo viwango vinavyohitajika, ni haki ya Wakenya kuuliza ni upungufu gani ambao umefanya Dkt Patrick Amoth wa Wizara ya Afya kukosa kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Afya wa nchi yake.

Kwa miaka kadhaa, isiyopungua mitatu, Dkt Amoth amekuwa kaimu mkurugenzi Mkuu wa Afya katika wizara ya Afya Kenya.

Licha ya kuonyesha viwango vya juu vya utaalamu na usimamizi hasa wakati wa janga la corona.

Dkt Amoth ameendelea kuwa kaimu mkurugenzi jambo ambalo linaibua maswali mengi kwa kuwa huo ni muda mrefu mtu kushikilia wadhifa bila kuthibitishwa.

Ni rahisi Wakenya kuamini kwamba Dkt Amoth ananyimwa haki yake hata baada ya kuhudumu chini ya mawaziri na makatibu kadhaa katika wizara hiyo.

Ikiwa ni utendakazi, ameteuliwa makamu rais wa Bodi Kuu ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) akiwakilisha bara la Afrika, dhihirisho kwamba anatambuliwa na kuheshimiwa kimataifa.

Huyu ni mtaalamu aliye na tajiriba kubwa hasa katika masuala ya usimamizi wa afya baada ya kupanda ngazi kutoka Afisa wa Afya katika Hospitali ya Mkoa ya Kisumu na iwapo kuna yeyote anayemnyima wadhifa wa Mkurugenzi wa Afya nchini hatendi haki.

Kushikilia ofisi ya mkurugenzi wa afya kwa zaidi ya mwaka hasa wakati wa janga kunaonyesha anaweza na kuna watu au mtu anayeweka vikwazo.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Miradi ya nyumba za bei nafuu ikamilishwe

CHARLES WASONGA: Ruto akabili ubadhirifu, ufisadi kufufua...

T L