• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
CECIL ODONGO: Kauli ya Kalonzo na Mudavadi ithibati hawana haja na ikulu

CECIL ODONGO: Kauli ya Kalonzo na Mudavadi ithibati hawana haja na ikulu

Na CECIL ODONGO

KAULI ya vinara wawili wa One Kenya Alliance (OKA), kuwa muungano wao hauna mbio kumteua mwaniaji wa Urais 2022, inaashiria kuwa hawana haja na kushinda kiti hicho hata wakifika debeni.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa ANC Musalia Mudavadi Jumamosi iliyopita, baada ya ibada katika kanisa la Nairobi East SDA, walishikilia bado kuna muda wa kutosha kabla ya kura hiyo na OKA haina haraka ya kutangaza mgombeaji wake.

Walionekana kumjibu Seneta wa Kakamega Cleophas Malala na baadhi ya wabunge wa ANC ambao mwezi jana, waliwapa masharti kuwa wawe wamemtaja mpeperushaji bendera wao kufikia Krismasi.Tamko la wawili hao linaashiria huenda wakaungana na ama kambi ya Naibu Rais au Dkt William Ruto kuelekea au baada ya uchaguzi huo wa 2022.

Huenda wanatathmini kuwania Urais kila mmoja kisha wawanyime Bw Odinga na Dkt Ruto kura chache ili mmoja wao asifikishe hitaji la kikatiba la kupata asilimia 51 ya kura zote. Kupitia ujanja huo, wataweka masharti ya kuingia kwenye mkataba wa kuunda serikali na mmoja wao kabla ya kuungana naye kwenye kampeni ya duru ya pili.

Kutetea usemi wao, wawili hao walirejelea kura ya 2002 ambapo uliokuwa muungano wa Narc ulimtaja Mwai Kibaki kama mgombeaji wake wa Urais miezi mitatu tu kabla ya uchaguzi kuandaliwa Disemba mwaka huo.Pia walirejelea, kura ya 2017 ambapo Kinara wa ODM Raila Odinga alitajwa kuwa mwaniaji wa kiti hicho kupitia NASA mnamo Aprili 27 ilhali uchaguzi ulikuwa Agosti 8.

Kwanza ni vyema Bw Musyoka na Mudavadi ambao walikuwa katika mrengo tofauti 2002 waelewe kuwa, matukio yaliyozingira kampeni ya mwaka huo yalikuwa tofauti na kura ya 2022.Mwaka huo hata kabla ya Bw Odinga kumtangaza Bw Kibaki kuwa mgombeaji wa Narc, tayari kiongozi huyo ambaye sasa amestaafu alikuwa na uungwaji mkono Mlima Kenya hata kuliko mpinzani wake mkuu Uhuru Kenyatta wa Kanu.

Isitoshe, pia alikuwa tayari kwenye muungano wa NAK ambao ulishirikisha Charity Ngilu (sasa Gavana wa Kitui) wa SDP wa marehemu Michael Wamalwa wa Ford Kenya.Wawili hao walikuwa na kura nyingi kutoka katika ngome zao na ujio wa kundi la Bw Odinga na waasi wengine wa Kanu kupitia LDP uliwaongezea nguvu zaidi.P

ia, mwaka huo Wakenya walikuwa wamechoshwa na utawala wa miaka 39 wa Kanu ambao uligubikwa na ukandamizaji wa wapinzani,. kunyima raia uhuru wa kujieleza na ufisadi tele na hayo yalichangia ushindi wa Bw Kibaki. Je, Bw Musyoka na Bw Mudavadi wana uungwaji mkono kama yaliyokuwa mawimbi ya Narc yaliyotikisa nchi 2002?

You can share this post!

Fahamu mengi kuhusu nyama ya sungura

Zetech ndio mabingwa wapya wa karate katika mashindano...

T L