• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 7:55 PM
CHARLES WASONGA: Ruto ajizatiti kukomesha ufisadi na ubadhirifu nchini

CHARLES WASONGA: Ruto ajizatiti kukomesha ufisadi na ubadhirifu nchini

NA CHARLES WASONGA

NILIFUATILIA kwa makini zaidi kikao cha kwanza cha Rais William Ruto na wanahabari katika Ikulu ya Nairobi ambapo alijibu maswali kadha kuhusu mipango yake ya kuboresha maisha ya Wakenya.

Dkt Ruto alijibu maswali kadha yanayohusu sekta mbalimbali za uchumi wa nchini kando na masuala kadha yanayokera zaidi na Wakenya kama vile kupanda kwa gharama ya maisha na ongezeko la bei ya stima.

Lakini kilichonishangaza ni kwamba Rais alikwepa kabisa kuelezea jinsi serikali yake itapambana na zimwi la ufisadi na ubadhirifu wa fedha serikalini.

Hii ni kwa sababu chunguzi nyingi zilizoendeshwa na asasi za kiserikali na zile za kibinafsi zimeonyesha kuwa, kwa wastani, serikali kuu hupoteza karibu Sh600 bilioni kila mwaka kupitia sakata mbalimbali za ufisadi.

Isitoshe, mnamo Januari 18, 2021, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alidai kuwa serikali yake ilikuwa ikipoteza Sh2 bilioni kila siku. Aliungama kuwa uovu huo ulikithiri katika Wizara, Idara na Mashirika (MDAs) za serikali, ikiwemo Afisi ya Rais.

Kwa kuwa Rais Ruto alihudumu kwa miaka 10 kama Naibu wa Bw Kenyatta, naamini kwamba anafahamu fika kwamba ufisadi ni mojawapo ya changamoto zilizodumaza juhudi za serikali iliyopita ya Jubilee kutimiza nyingi ya ahadi zake kwa Wakenya.

Mojawapo ya ahadi hizo ni utekelezaji wa mpango wa utoaji tarakilishi tamba kwa wanafunzi wa darasa la kwanza kuanzia 2013.

Nashuku kuwa huenda baadhi ya ahadi ambazo Rais Ruto alitoa kwa Wakenya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 huenda zikakosa kutekelezwa ilivyotarajiwa kutokana na uovu huu wa ufisadi.

Aidha, japo Rais Ruto na wandani wake wamekuwa wakidai kuwa walirithi serikali ambayo ilikuwa fukara, wamekuwa wakiendeleza matumizi mabaya ya fedha za umma.

Itakumbukwa kuwa alipoingia mamlakani Septemba 13, 2022 Rais aliahidi kupunguza bajeti ya kitaifa ili kuokoa Sh300 bilioni alizoahidi kwamba zitaelekezwa katika masuala yanayohitaji udharura kama vile mipango ya kukabiliana na njaa.

Aidha, mnamo Novemba 1, Wizara ya Fedha ilipiga marufuku mienendo ya maafisa wa serikali kufanya mikutano na warsha katika mikahawa ya kifahari ya kibinafsi ili kuokoa pesa za umma.

Iliagiza kuwa mikutano kama hiyo ifanyiwe katika majumba ya serikali ambako serikali haitagharamika kulipia ada ya kukodisha kumbi za mikutano.

Kwenye taarifa iliyotiwa saini na Waziri Profesa Njuguna Ndung’u, serikali pia ilipiga marufuku ziara za kila mara za maafisa wa serikali katika mataifa ya ng’ambo, ili kupunguza matumizi ya pesa za umma.

Lakini kinaya ni kwamba agizo hilo limeendelea kukiukwa na viongozi wakuu wa serikali na bado wanaendelea kufanya mikutano yao katika mikahawa ya kibinafsi.

Mfano mzuri ni mkutano wa mawaziri, makatibu wa wizara na maafisa wakuu wa serikali ulioandaliwa katika mkahawa wa kibinafsi wa Fairmont Mount Kenya Safari Club, ulioko Nanyuki, Kaunti ya Laikipia.

Mkutano kama huo, ungefanyika katika Ikulu ya Ndogo ya Sagana iliyoko katika kaunti jirani ya Nyeri na hivyo serikali ingeokoa fedha nyingi zaidi.

  • Tags

You can share this post!

WANGU KANURI: Rais ahakikishe wanafunzi kote nchini...

TAHARIRI: Ukame: Dua pekee si jibu bali teknolojia

T L