• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 8:22 PM
TAHARIRI: Ukame: Dua pekee si jibu bali teknolojia

TAHARIRI: Ukame: Dua pekee si jibu bali teknolojia

NA MHARIRI

UKAME ambao unaendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo nchini umesababisha njaa na mahangaiko tele.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa zaidi ya Wakenya milioni 4 wanahitaji msaada wa chakula kwa dharura na Shirika la Umoja wa Kimataifa (UN) limeonya kuwa makali ya njaa humu nchini yataendelea kwa miezi kadhaa ijayo.

Baa la njaa limegeuka kuwa donda ndugu nchini Kenya – kwani limekosa suluhisho. Kila mwaka mamilioni ya Wakenya wanalilia msaada wa chakula.

Uhaba wa chakula nchini unasababishwa na ukosefu wa mvua. Hii inatokana na ukweli kwamba Kenya hutegemea mvua kwa asilimia 99 katika uzalishaji wa chakula.

Kila mara ukame unapobisha hodi, viongozi wa kidini na kisiasa wanakimbilia kuandaa mikutano ya maombi kumsihi Mungu kuleta mvua. Kiongozi wa hivi karibuni kuandaa maombi ni Naibu wa Rais Rigathi Gachagua ambaye juzi aliombea mvua huku akitazama Mlima Kenya.

Akiwa katika ufuo wa Mto Rikki, Kaunti ya Nyeri, alipokuwa akielekea kuomba, Bw Gachagua alisema kuwa huu ni ukame mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa ndani ya miongo minne iliyopita.

Mkewe Bw Gachagua, Bi Dorcas Gachagua, pia akiwa Kaunti ya Makueni mnamo Oktoba mwaka uliopita aliombea mvua baada ya kujionea jinsi ukame na ukosefu wa chakula ulivyowaathiri maelfu ya wakazi.

Viongozi wa Kiislamu katika maeneo mbalimbali ya nchi pia wamekuwa wakiandaa mikutano ya maombi kusihi Allah (Mungu) kuleta mvua.

Japo maombi ni mazuri, serikali haina budi kuchukua hatua zaidi ya kumlilia Mungu kuleta mvua. Ukame unaoshuhudiwa nchini ni matokeo hasi ya mabadiliko ya tabianchi. Si Kenya pekee ambayo imeathiriwa na mabadiliko ya tabianchi bali ni changamoto ya ulimwengu mzima.

Maombi pekee hayataweza kubadili mabadiliko hayo. Mungu ameipa nchi rasilimali na maarifa tele tunayoweza kuyatumia kukuza chakula cha kutosha bila kutegemea mvua.

Hatua ya serikali kutoa mbolea nafuu kwa wakulima pekee haiwezi kumaliza tatizo la baa la njaa ambalo hushuhudiwa nchini kila mwaka.

Serikali haina budi kuwezesha wakulima kukumbatia teknolojia katika kilimo. Ukweli ni kwamba asilimia 80 ya chakula kinachozalishwa nchini kinatokana na wakulima wa mashamba madogo ambao wengi wao wanatumia mbinu zilizopitwa na wakati katika ukulima.

Juhudi za Rais William Ruto kujaribu kuboresha kilimo cha unyunyiziaji katika eneo la Galana Kulalu ni habari njema.

Mradi huo wa Galana Kulalu ukisimamiwa vyema utasaidia pakubwa kupunguza idadi ya waathiriwa wa njaa kila mwaka.
Aidha, sidha, serikali inafaa kuongeza idadi ya miradi ya ukulima ya unyunyiziaji katika meneo mbalimbali ya nchi kuwezesha nchi kuwa na chakula cha kutosha.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Ruto ajizatiti kukomesha ufisadi na...

Covid-19: Furaha China ikifungua mipaka yake

T L