• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
DOUGLAS MUTUA: Vijana wafundishwe vya bwerere havitoshi kitu

DOUGLAS MUTUA: Vijana wafundishwe vya bwerere havitoshi kitu

NA DOUGLAS MUTUA

WANAFIKI wa mtandaoni hawatupi fursa tukapumua wakitupa ushauri, ambao kamwe hatukuwaomba, kuhusu maadili ya kimaisha. 

Wanalaani maovu wanayoshiriki gizani.

Wanapiga mfano wa marehemu Fridah Warau Kamuyu, 23, msichana aliyekufa maji pamoja na anayedhaniwa kuwa mpenzi wake eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu.

Fridah na Tirus Maina Gikonyo, mume wa mtu aliyeaminika kuwa na jicho la nje, walifariki katika hali ya kutatanisha pale gari la Gikonyo lilipozama kwenye bwawa la Titanic.

Sasa wawili hao wametangulia mbele ya haki na miili yao ikazikwa, lakini wanaojiona mafundi wa maadili hawaishi kutusumbua kwa maneno ya ‘umuhimu wa kuwanasihi vijana’.

Kwa maoni ya watu hao wanaopenda kuona vibanzi vilivyo ndani ya macho ya watu na wala si maboriti yaliyomo machoni mwao, vijana wa siku hizi hawana mwelekeo.

Wanawalaumu vijana kwa kupenda maisha ya kuponda mali bila kuyafanyia kazi; wavulana wanawekwa rumenya, wasichana ndio nyumba ndogo eti.

Kisa na maana hawapendi kuchoka, wanataka kumaliza masomo ya sekondari, kuingia mijini na kukumbana na mafedha yasiyoisha. Watayapata wapi isipokuwa kwa wale waliovumilia masaibu mengi kitambo wafikie hapo? Wengi walio nazo tele benkini ni watu wazima na familia zao.

Katika zile juhudi za ‘kujishukuru’ kwa kufanya kazi kwa bidii, tajiri anajisadikisha kwamba hajafikishwa alipo na maadili, hivyo “paka mzee anakunywa maziwa tu”.

Mtazamo wa wadaku wa mtandaoni kuhusu vijana wa siku hizi unaweza kuwa na ukweli fulani, lakini binafsi sikubaliani nao kwa sababu unahukumu kizazi kizima cha vijana.

Wapo vijana wanaozingatia maadili waliyopata kutoka kwa wazazi wao na dini, hivyo utawapata ofisini au viwandani wakifanya kazi nzuri walizosomea.

Nina ushahidi wa vijana kadhaa waliojiunga na kazi ya uanahabari yapata miaka 10 iliyopita, mara tu baada ya kuhitimu vyuo vikuu, na sasa ni wahariri bingwa. Kuna vijana wa umri wa chini ya miaka 30 ambao wanamiliki biashara kubwa, wasiolala usingizi wa kutosha kwani usiku wanahesabu hela na kupanga mikakati ya kufaulu.

Kipo kizazi cha vijana waliogundua umuhimu wa kuwekeza katika uchakataji wa bidhaa viwandani na wanauza bidhaa hizo ndani na nje ya nchi.

Hao hawana haja kuwafuata wake na waume wa watu wenye mafedha ili angaa shilingi mbili-tatu zikianguka waokote na kulipa kodi za nyumba.

Baadhi yao watakushangaza wakikuhadithia historia zao. Baadhi yetu tuliamini hadithi aliyotamba Charlene Ruto, binti wa Rais wa Kenya, kwamba aliwauzia wanafunzi wenzake bidhaa za kawaida alipokuwa chuoni.

Wengi waliosikia hadithi hiyo walisema haingaliwezekana kwa binti wa naibu rais (wakati huo) kuwa mchuuzi wa bidhaa duni, eti anapaswa kulishwa kama mtoto chumbani.

Ngoja nikufichulie siri ya matajiri: wanaotaka utajiri wao urithiwe na vizazi hata vizazi huwafundisha watoto wao kutafuta mali, si kuiponda.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Namwamba, viongozi nchini wasaidie klabu za soka...

WANDERI KAMAU: Naam, Ruto anafanya vyema kuzima miungano ya...

T L