• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
KAMAU: Uchawi: Tamaduni za jadi zinadunisha jamii

KAMAU: Uchawi: Tamaduni za jadi zinadunisha jamii

Na WANDERI KAMAU

WAKATI huu ambapo dunia inashuhudia mabadiliko mengi ya kiteknolojia, ni vigumu kudhani kizazi cha sasa kinaweza kushabikia na kuendeleza baadhi ya tamaduni ambazo ziliendelezwa katika nyakati za mababu zetu.

Bila shaka, mabadiliko yanayoendelea yanapaswa kukifungua macho kizazi hiki kufahamu kuwa hakipaswi kuachwa nyumba dunia inapoendelea kubadilika.

Miongoni mwa masuala kinachopaswa kuyaangazia upya ni mtindo wake wa kimaisha, mtazamo mpya kuihusu dunia, maingiliano ya watu na tamaduni zao, miegemeo ya kidini, mitazamo yao kuhusu jinsia kati ya masuala mengine muhimu.

Licha ya teknolojia kutoa nafasi kwa kila mmoja kuwa sehemu ya mabadiliko yanayoendelea, inasikitisha kuwa baadhi ya vijana barani Afrika wameamua kukwamilia katika ukale na tamaduni dhoofu ambazo hazina maana yoyote katika maisha ya kisasa.

Mifano halisi ya ‘ukale’ huo ni mtindo wa baadhi ya vijana kuwachoma na kuwashambulia wazee kwa kisingizio cha kuendeleza uchawi na ushirikina.

Katika siku za hivi karibuni, wazee wameripotiwa kuishi kwa hofu, hasa katika maeneo ya Kisii, kwani jamii hiyo inaonekana kubuni mtazamo na dhana kwamba wengi wao ni wachawi.

Katika mila za Kiafrika, uchawi ulikuwa kama njia ya jamii fulani kujilinda dhidi ya kukumbwa na mikosi.

Hivyo, haikuwa makosa yoyote kwa wachawi kuwepo, bali kosa lilikuwa kuutumia kumdhuru mtu ama watu.

Mitazamo kuhusu wachawi na waganga ilianza kubadilika wakati wamishenari walifika Afrika na kuanza kuzifunza jamii hizo kuhusu dini kama Ukristo na Uislamu.

Kulingana na mafundisho ya wamishenari hao, uchawi na uganga ulikuwa “njia na vitendo vya kishetani”.

Hivyo, wale walioendesha masuala hayo mawili walikuwa “maajenti” wa kishetani.

Kutokana na mafundisho hayo, jamii nyingi zilianza kuwachukia waganga na wachawi, licha ya michango yao kuwa muhimu katika maisha ya awali ya jamii hizo.

Bila shaka, nyakati zimebadilika, ambapo ni vigumu sana kwa sasa kumsikia mtu akirejelea imani za kichawi ama uganga kuchangia “ufanisi” wake katika masuala fulani.

Kinyume na ilivyokuwa zamani, kuna vumbuzi za kisayansi zinazotumiwa kutibu baadhi ya maradhi yaliyoaminika kutokuwa na tiba.

Vile vile, kuna imani za kisasa za kidini ambazo zimefifisha sana dhana za uchawi na uganga miongoni mwa jamii zetu.

Katika mazingira yanayotawaliwa na usasa, ni makosa kwa yeyote kumdhuru mtu kwa kisingizio cha kuendeleza uchawi, uganga au ushetani.

Maswali yanayoibuka ni: Ni vigezo vipi wanazotumia wale wanaowashambulia wazee ili kubaini wanaendeleza maovu hayo? Kuna nguvu ama uwezo maalum walio nao?

Bila shaka, visa hivyo ni uhalifu na kukosa utu. Wahusika wanapaswa kushtakiwa na kuadhibiwa vikali kwani hakuna mtu anayeruhusiwa kisheria kumwadhibu mwenzake kwa namna yoyote ile.

Kwa kauli hii, simaanishi visa na vitendo vya uchawi na ushirikina havipo. La hasha! Vipo kwa vingi.

Hata hivyo, taratibu za kisheria zinapaswa kufuatwa kuchunguza na kubaini ikiwa ni kweli washukiwa wanaendesha maovu hayo au la.

Wakati pia umefika kwa kizazi cha sasa kujikomboa kutoka kwa baadhi ya tamaduni na itikadi za kikale ambazo daima zinakirudisha nyuma.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Ogoti azimwa kusikiza kesi dhidi ya gavana Njuki na mkewe

Jaji mkuu kuapisha majaji sita endapo Rais Uhuru Kenyatta...

T L