• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 1:12 PM
NGILA: Jina jipya la Facebook liambatane na maadili

NGILA: Jina jipya la Facebook liambatane na maadili

Na FAUSTINE NGILA

FACEBOOK imebadilisha jina. Kwa sasa inaitwa Meta, kampuni ambayo itasimamia biashara ya huduma za Facebook, Instagram, WhatsApp, Messenger na Oculus.

Kama tu ilivyofanya Google hapo 2015 ilipojiita Alphabet, kwa kujiita Meta, Facebook imesema inanuia kuboresha huduma zake kwa watumizi na kuwaandaa kwa mustakabali wa huduma za intaneti kijumla.

Hata hivyo, wengi wamesema kuwa huenda Facebook imebadilisha jina ili kujiondolea sifa mbovu ambazo zimeiandama katika miaka ya hivi majuzi, jinsi ilivyofanya Barclays kujiita Absa.

Katika juhudi zake za kujizolea faida ya mabilioni katika biashara ya matangazo ya mitandaoni, Facebook imejipata taabani hasa kutokana na matumizi ya data za siri za wateja bila idhini.

Kwa kujiita Meta, Facebook sasa inalenga kuendeleza matumzi ya data hizi, kwa vile inaviita vifaa vya kuwaletea wateja huduma za video zinazoleta matukio kwa mbashara.

Kumekuwa pia na ripoti kadhaa kuhusu jinsi mtandao wa Facebook unaeneza habari feki hasa katika kipindi cha janga la corona na kuchangia kwa vifo vya maelfu ya watu walioamini ushauri wa kishenzi kuhusu tiba ya ugonjwa huo.

Ripoti zilizotolewa wiki iliyopita pia zilianika jinsi mtandao huo unavyotumika na wauzaji wa dawa za kulevya, biashara hatari sana kwa uchumi wa dunia.

Pia, kumekuwa na tetesi kuwa huduma za Facebook na Instagram zimetumika katika ulanguzi wa binadamu kote duniani, uovu ambao unavunja haki za kibinadamu.

Isitoshe, mitandao yake ya kijamii imetumika kueneza chuki wakati wa kampeni za chaguzi kadhaa duniani, ambapo wanasiasa hulipia matangazo yenye jumbe za kudhalilisha washindani wao na kuchochea ghasia za kabla na baada ya uchaguzi miongoni mwa wafuasi.

Usisahau pia kuwa Facebook inaongoza kwa dhuluma za kimitandaoni kulingana na tafiti mbalimbali ambazo nimezisoma, huku wanawake wakiumia zaidi kutokana na dhuluma za kijinsia na kimapenzi kule mitandaoni.

Majuzi, Instagram ilijipata motoni kwa kudai kanuni zake za kulinda hazifai kukosolewa, licha ya kuruhusu matini ambayo hayafai kwa watu wa umri mdogo.

Ingawa pia kampuni hiyo imeinua biashara ndogo ndogo kwa kuzipa majukwaa ya kuuza bidhaa zao mitandaoni bila malipo, labda kubalilisha jina kuwa Meta ni fursa mwafaka ya kubadilisha pia sifa mbaya ambazo zinahusishwa nayo.

Ni wakati wa Meta sasa kubadilisha mwonekano wa ndani na nje ya kampuni hiyo, na sasa kuchukulia usiri wa data kwa uzito unaofaa.

Meta inafaa kujua kuwa licha ya huduma zake kupendwa na wateja wake, inafaa kuwa katika mstari wa mbele katika kulinda usalama wao mitandaoni.

Hii haifai kuwa njama fiche ya kunyonya data za siri za wateja.

Meta isijifiche ndani ya teknolojia za kisasa ili kuchukua data za watumizi na kuruhusu kampuni zenye sifa za Cambridge Analytica kuiba data na kuichanganua kwa niaba ya wanasiasa.

Iwapo Meta ina hakika inataka kuunda mustakabali wa huduma za intaneti, basi inafaa kuanza kuzingatia mambo ya kimsingi ya kuwalinda wateja wake.

Tusisikie tena kuwa binadamu wanauzwa kwenye mtandao huo, habari za dhuluma zikome, ripoti za kuruhusu mauzo ya mihadarati zitamatishwe na wala tusione jumbe za chuki zikienezwa tena.

  • Tags

You can share this post!

WASONGA: Vinara wa OKA wanawakanganya wafuasi wao

Serikali irejeshe spoti shuleni – Kuppet

T L