• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 6:50 AM
Serikali irejeshe spoti shuleni – Kuppet

Serikali irejeshe spoti shuleni – Kuppet

Na DERICK LUVEGA

MUUNGANO wa Walimu wa Sekondari nchini (Kuppet) umetoa wito kwa serikali kurejesha shughuli za spoti shuleni kama njia ya kukabiliana na hali ya wanafunzi kuchoma mabweni.

Katibu mkuu wa muungano huo, Sabala Inyeni, alisema kurejeshwa kwa shughuli za michezo hizo zilizopigwa marufuku kutokana na janga la corona itasaidia kupunguza visa vya wanafunzi kuchoma mabweni na kuharibu mali ya shule.

“Baadhi ya wanafunzi wanahisi kuwa wafungwa. Tunaomba serikali irejeshe michezo ya mashindano ili kupunguza visa kama hivyo,” akasema Bw Inyeni.

Mpango huo ulioanza mwaka 2020 umewafanya wanafunzi kukaa shuleni kwa muda mrefu ili kufidia muda uliopotea wakati shule zilipofungwa kwa takriban miezi tisa kutokana na corona.

“Haya yasipokomeshwa, mtihani wa kitaifa utakaofanywa mwaka ujao utaathiriwa. Serikali inafaa kuwapa wanafunzi siku chache kupumzika. Wanafaa kushiriki katika shughuli za nje kama vile mchezo. Tangu spoti kupigwa marufuku miongoni mwa wanafunzi wa sekondari, visa vya maandamano na mabweni kuchomwa vimekuwa jambo la kawaida nchini.”

Alisema kuwa muhula huu hauna mapumziko na wanafunzi wanaweza kusababisha machafuko ili wapate siku chache za kurudi nyumbani.

Aliomba serikali kutoa fedha za kufadhili shughuli za michezo baina ya wanafunzi hata wakati wakuu wa shule wakiandaa mipango ya shughuli za shule.

Kwingineko, viongozi wa dini chini ya jukwaa la Ushauri la Dini, Kaunti ya Vihiga wanaiomba serikali kuwateua wataalamu na makasisi watakaowapa wanafunzi ushauri wakiwa shuleni.

You can share this post!

NGILA: Jina jipya la Facebook liambatane na maadili

Koome aagiza mahakama zianze kusikiliza kesi kwa njia ya...

T L