• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 10:50 AM
TAHARIRI: IEBC iwatoe shaka wananchi kuhusu mgeni kumiliki vifaa vya uchaguzi

TAHARIRI: IEBC iwatoe shaka wananchi kuhusu mgeni kumiliki vifaa vya uchaguzi

NA MHARIRI

MZOZO unaoendelea kuhusu kukamatwa kwa mshukiwa kutoka Venezuela akiwa na vifaa vya uchaguzi unahitaji ufumbuzi wa haraka.

Tukio hilo la Ijumaa limezua maswali mengi huku polisi, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) na viongozi wa Kenya Kwanza wakiwa kwenye mjadala mkali.

Punde tu raia huyo wa Venezuela, Jose Gregorio Camargo Castellanos alipokamatwa, Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati aliandika taarifa akisema kuwa polisi walimshika mfanyikazi wa IEBC.

Uchunguzi uliofanywa na DCI unaonyesha kuwa baada ya kuhojiwa, Jose alikiri kuwa hakuwa mfanyikazi wa IEBC wala siyo iliyomwalika nchini, bali mtu aliyemtaja kuwa Abdulahi Abdi Mohamed.

Pia, alikiri kuwa vifaa vya uchaguzi vya kaunti 11, laptop, flashi, simu na vifaa vingine vya kutumika na kompyuta vilikuwa mali yake na wala si ya IEBC.

Hata kama kweli DCI wanasema uongo kama alivyodai Naibu Rais William Ruto baadaye jana Jumapili, basi hebu Bw Chebukati na IEBC wajibu maswali haya: Kama aliyekamatwa ni mfanyikazi wa kampuni ya Smartmatic International Holding B.V ambayo iko London, ni kwa nini mshukiwa alitoka na vifaa Panama, akapitia Uturuki na kutua Nairobi?

Kampuni ya Smartmatic ndiyo iliyo na mkataba wa kusambaza vifaa vya KIEMS vya uchaguzi. Kama ni hivyo, mbona vifaa vilivyokuwa kwenye mikoba ya Jose havikuwa na anwani ya kupelekwa kwa IEBC? Au ina maana kuwa vilikuwa salama zaidi mikononi mwa raia huyo wa kigeni kuliko maafisa wa shirika la ndege?

Mbona masanduku ya karatasi za kura hutumwa kwa ndege hizo hizo na huandikwa vizuri kuwa ni mali ya IEBC? Mbona hakuna hata mfanyikazi mmoja wa IEBC aliyefika uwanjani kupokea mzigo wao?

Maswali ni mengi lakini cha msingi hapa ni kuwa uchaguzi wa Kenya na Afrika kwa jumla huwa suala la uhai na mauti.

Wanasiasa huwa wametumia mamilioni ya pesa zao na za wanaowafadhili, na hutarajia kushinda wala si vinginevyo.

Kwa sababu hiyo, wanasiasa hutumia kila mbinu watangazwe washindi.

Ili mtu akubali kuwa kweli ameshindwa, ni lazima wanaosimamia uchaguzi wathibitishe kuwa kweli shughuli yote ya uchaguzi, kuanzia maandalizi, ilikuwa huru na ya haki.

Uchaguzi una wadau wengi. Mbali na wawaniaji na IEBC, kuna maafisa wa usalama na Tume ya Mawasiliano (CA) inayofanya kazi na kampuni za simu, ili kuwe na mtandao wa kupeperushia matangazo.

Lakini wadau wakubwa ni wapiga kura. Hakuna anayepoteza muda kwenda kituoni ikiwa hana uhakika kama kura yake itahesabiwa.

You can share this post!

Familia ya Kangogo yataka uchunguzi kuhusu kifo chake...

Wagombea urais waingia baridi kuhusu mdahalo

T L