• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 2:54 PM
Wagombea urais waingia baridi kuhusu mdahalo

Wagombea urais waingia baridi kuhusu mdahalo

NA MARY WANGARI

WASIWASI unakumba kikao cha mdahalo wa waniaji urais kesho Jumanne, baada ya wawaniaji watatu kutilia shaka maandalizi.

Mwaniaji urais wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila Odinga, ndiye wa hivi punde kutangaza kutoshiriki baada ya mpinzani wake mkuu, kiongozi wa Kenya Kwanza, Naibu Rais William Ruto, kutishia kususia akilalamikia kuhusu “ubaguzi wa vyombo vya habari.”

Hata hivyo, mnamo Alhamisi, Dkt Ruto alionekana kubadili nia na kutangaza kupitia sekretariati yake ya kampeni za urais, kuwa atashiriki mdahalo huo.

Kupitia msemaji wake Bw Hussein Mohamed, Dkt Ruto alitoa masharti kwa waandalizi waeleze walivyotenga muda wa kujadili masuala muhimu kama vile elimu, uchumi, ufisadi, afya na mengineyo.

Jana Jumapili Bw Odinga kupitia msemaji wa Kampeni zake za Urais, Profesa Makau Mutua, alisema hatoshiriki mdahalo huo kwa sababu hautajadili masuala muhimu yanayowaathiri Wakenya.

“Dkt Ruto amesisitiza kuwa mdahalo usiangazie ufisadi, uadilifu, maadili na utawala, masuala makuu yanayowakabili Wakenya. Masuala haya ni msingi wa kampeni za Azimio. Mdahalo wowote usiojadili masuala haya ni dhihaka kwa Wakenya,” ilisema taarifa.

Gavana wa Laikipia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kampeni za Azimio, Ndiritu Muriithi, vilevile amesema kiongozi wa ODM amejiondoa katika mdahalo huo ili kumnyima nafasi Naibu Rais ya kuwahadaa Wakenya.

“hatufikiri tunapaswa kushiriki shughuli itakayoishia kuwalaghai Wakenya. Washindani wetu wamekuwa wakichukua ukweli na kuugeuza ili kufanikisha malengo yao kisiasa na hatufikiri hivyo ni sawa,” alisema gavana Muriithi.

Badala yake, Bw Odinga alisema wataandaa kikao katika Ukumbi wa Jericho, Eastlands, Nairobi, ambapo pamoja na mgombea mwenza wake Martha Karua watakutana na wananchi na kuzungumzia matatizo yanayowakabili.

“Kampeni yetu imesafiri nchi kukutana na wapiga kura na kusikiza changamoto zao, na kwa kufanya hivyo kutafuta suluhisho na Wakenya wote. Kwa kawaida, midahalo hutoa fursa sawa na hiyo kwa wapigakura kusikia moja kwa moja kutoka kwa wagombea na kuamua ikiwa wawaniaji wanatimiza maadili yao,” alisema.

Kiongozi wa Roots Party, George Wajackoyah vilevile ametishia kutohudhuria mdahalo wa kitaifa akilalamikia kuhusu mpangilio wake anaosema unawabagua washiriki.

Kulingana na ratiba, Bw Wajackoyah amepangiwa kukabiliana na kiongozi wa Agano Party, David Mwaure, katika awamu ya kwanza kwa msingi kwamba, kura ya maoni inaonyesha kiwango cha umaarufu kwa wote wawili ni chini ya asilimia 5.

Katika awamu ya pili, Dkt Ruto atamenyana na Bw Odinga, kwa sababu umaarufu wao ni zaidi ya asilimia tano.

Prof Wajackoya amesisitiza kuwa atahudhuria mdahalo huo ikiwa tu, atakabiliana na wawili hao, akisema kura ya maoni iliyotumika kupanga ratiba haina msingi.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: IEBC iwatoe shaka wananchi kuhusu mgeni kumiliki...

DCI yapaka tope IEBC kura ikibisha

T L