• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 5:55 PM
TAHARIRI: Jamii itajuta kuvumilia wahalifu walio kwa bodaboda

TAHARIRI: Jamii itajuta kuvumilia wahalifu walio kwa bodaboda

NA MHARIRI

WAKATI uchukuzi wa umma kwa njia ya pikipiki ulipoanza kuvuma miaka michache iliyopita, haingetarajiwa kwamba sekta ya bodaboda ingebadilika kuwa ya maovu tele katika jamii.

Kisa ambacho kilishuhudiwa jana Nairobi ambapo mwanamke alivamiwa akadhulumiwa mchane peupe na watu wanaoaminika kuwa wahudumu wa bodaboda, kinafaa kuzindua wadau wote walio na jukumu la kudhibiti sekta hiyo kutoka usingizini.

Ingawa kuna wahudumu ambao hufuata sheria wanapojitafutia riziki, hatuwezi kamwe kufumbia macho maovu ambayo yamekuwa yakihusishwa na sekta hiyo kwa muda mrefu sasa.

Maafisa wa usalama huwa wamewahi kukiri kwamba kuna wahalifu wanaojificha ndani ya wahudumu wa bodaboda ila juhudi ambazo hutangazwa kila mara kujaribu kuwaondoa hazionekani kufua dafu.

Mara nyingi wananchi wamejionea wahalifu wanavyojifanya kuwa wanabodaboda wakipora watu, wengine wao wakiwa hata wamejihami kwa bunduki.

Katika maeneo ya mashinani, vijana wanaofanya kazi hiyo ndio hulaumiwa sana kwa kuhadaa watoto wa kike na kuwashikisha mimba wengine wao wakiwa bado ni wanafunzi wa shule za msingi.

Kando na hayo, ni sekta hii pia ambapo ajali inapotokea kati ya gari na mhudumu wa bodaboda, unaweza ukachomewa gari lako na wewe mwenyewe ukapigwa hata kama kosa si lako.

Haya ni mambo ambayo, kusema kweli, yamepuuzwa kwa muda mrefu na hayastahili kuendelea kuvumiliwa.

Sekta ya bodaboda inakua kwa kasi katika kila pembe ya nchi hasa kutokana na jinsi ilivyo rahisi kwa vijana kuingilia biashara hiyo ikilinganishwa na kutafuta aina nyingine za vibarua.

Hii ni kumaanisha kuwa, huenda kukawa na changamoto zaidi ya jinsi ilivyo kwa sasa katika siku za usoni kwani inatarajiwa sekta hiyo itaendelea kupanuka.

Wakati mdahalo unapoendelea kuhusu hitaji la kudhibiti huduma za bodaboda, ni muhimu pia wadau wote kutafuta mbinu za kuletea vijana aina nyingine za ajira.

Hivi sasa serikali ya kitaifa na baadhi ya kaunti huwa zimetenga fedha za kufadhili masomo ya vijana katika taasisi za kiufundi, lakini imebainika vijana wengi huchagua bodaboda badala ya kuendea masomo hayo.

Kuwapa vijana uwezo wa kujiendeleza kimaisha pia kutachangia kupunguza idadi ya wanaojitosa katika bodaboda, na hivyo basi kurahisisha mbinu za kudhibiti sekta hiyo ili kuondoa wahalifu wanaojificha ndani yake.

You can share this post!

Ni KCPE kwa hofu vijiji vikichomwa kaunti ya Baringo

Anaamini ana kipaji cha kufanya vizuri na kutinga upeo wa...

T L