• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
TAHARIRI: Kuhubiri chuki ya kisiasa tishio kwa taifa kabla ya kura

TAHARIRI: Kuhubiri chuki ya kisiasa tishio kwa taifa kabla ya kura

Na MHARIRI

SIKU ya Jumamosi kuliandaliwa mkutano mkubwa sana katika uwanja wa Eldoret Sports Club.

Mkutano huu ulikuwa wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Naibu Rais Dkt William Ruto.

Azma kuu ya mkutano wa Jumamosi ilikuwa fursa ya wenyeji wa ngome anakotoka Naibu Rais pamoja na wazee kumpa baraka anapojiandaa kuzama kikamilifu katika kampeni za kuwania urais mwaka huu.

Ni katika majukwaa kama haya ambapo wengi wa viongozi wenye ndimi za upanga hujisahau hasa wanapopandwa na pepo wa kisiasa. Na kwa kweli Jumamosi haikuwa tofauti.

Wanasiasa mbalimbali walipopanda jukwaani kumpa Naibu Rais sifa kedekede na kumwombea kila la kheri katika safari yake ya kutaka kuingia Ikulu, zamu ya Mithika Linturi ilipowadia watu wengi walishtuka.

Linturi aliwataka wakazi wa eneo la Bonde la Ufa kuhakikisha kwamba katika uchaguzi wa Agosti wanayafagilia mbali ‘magugu’ yote katika ngome ya Naibu Rais. Ingawa ni sawa kuwashawishi wapigakura kupiga kura kwa namna fulani, seneta Linturi anafaa kukumbushwa kwamba eneo alikotolea matamshi haya fasiri ya neno ‘magugu’ ina maana tofauti na aliyoilenga.

Katika chaguzi za miaka ya 19992, 1997 na 2007/08 lugha kama hii ilipotumiwa ilimaanisha watu wasio na asili ya wenyeji wa Bonde la Ufa walifaa kufurushwa. Ni baada ya chaguzi hizi ambapo lugha hii ya kimafumbo ilisababisha watu wasio wenyeji kuteketezewa mali, kufurushwa katika makao yao na hata kuuawa.

Neno ‘madoadoa’ katika eneo la Bonde la Ufa ni neno linaloibua hisia kali. Na maadamu Linturi ni mwanasiasa wa muda mrefu anafaa awe analifahamu hili. Ghasia za baada ya uchaguzi zikitokea katika eneo hili atakuwa ni mmoja wa watakaolaumiwa.

Hata ingwa miongoni mwa wandani wa Naibu Rais Linturi alieleweka kwamba alilenga wanasiasa wasiomuunga mkono kama vile Alfred Keter, Silas Tiren, Swarup Mishra, Joshua Kutuny na Margaret Kamar, anafaa akumbushwe kwamba Kenya ni nchi huru inayozingatia demokrasia na hivyo watu wako huru kuwa na misimamo tofauti ya kisiasa.

Naibu Rais anafaa kukashifu matamshi haya ya mwendani wake kwa sababu ni mara nyingi amekuwa akitetea haki ya watu kujieleza licha ya misimamo yao ya kisiasa.

Uchaguzi wa Agosti unaponukia kauli kama hizi hazifai kupuuzwa. Viongozi wa namna hii mbali na kufaa kuchukuliwa hatua na vyombo vya dola, wanafaa wakataliwe mbali na wapigakura katika uchaguzi mkuu.

Linturi na wenzake wenye hulka sawa, ni maadui wa ustawi wa demokrasia, uwiano na utangamano wa kitaifa ambao tunahitaji ili kupiga hatua kimaendeleo.

You can share this post!

Beki Axel Tuanzebe ajiunga na Napoli ya Italia kwa mkopo

Watu wawili wauawa Lamu genge hatari likitekeleza unyama...

T L