• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
TAHARIRI: Maelezo kuhusu wawaniaji wote yaanikwe wazi

TAHARIRI: Maelezo kuhusu wawaniaji wote yaanikwe wazi

NA MHARIRI

MJADALA kuhusu vyeti vya masomo vya wanasiasa unazidi kuibua hisia mseto baina ya wananchi wakati huu ambapo maandalizi ya Uchaguzi Mkuu yanaelekea kileleni.

Kwa muda mrefu, suala hili limekuwa likizungumziwa huku vyeti ambavyo baadhi ya wanasiasa wanatumia kuingia mamlakani vikitiliwa shaka.

Ingawa hitaji la wanasiasa kuthibitisha kuwa stakabadhi zao ni halali kabla ya kuzipeleka kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ili waidhinishwe kuwania viti mwaka huu linatazamiwa kusaidia kuepusha uwasilishaji wa stakabadhi ghushi, bado kuna hatua zaidi ambazo zinafaa zichukuliwe kuziba mianya yote ya ulaghai.

Itakuwa vyema kama kutakuwa na sera au sheria ya uchaguzi kwamba, maelezo muhimu aina hii kuhusu wanasiasa wote yaanikwe wazi kwa umma ili waweze kujifanyia upekuzi wenyewe kwa njia huru.

Kufikia sasa, kuna maeneo ambapo wananchi hawajui chochote kuhusu kiwango cha masomo cha wawaniaji ugavana, ilhali katika eneo hilo hilo, kuna wawaniaji ugavana ambao kisomo chao kimeibua gumzo kitaifa kwa kiasi cha kuvutia upelelezi wa kihalifu dhidi yao.

Machoni pa umma, mwanasiasa anayechunguzwa hata kama hajapatikana na hatia huonekana kuwa ana doa.

Itakuwa ni haki tu ikiwa maelezo kuhusu wanasiasa wote yataanikwa wazi ndipo raia wapate nafasi ya kuweka maelezo hayo kwenye mizani, na kufanya utathmini kubainisha ukweli kuhusu wanasiasa wanaotaka kuwaongoza.

Suala hili la masomo sasa halichukuliwi tu kama mbinu ya kujua kiwango cha elimu cha kiongozi, bali limegeuka kuwa suala la uadilifu.

Pindi tu jambo lolote lile linapoanza kuvutia ulaghai jinsi tunavyoshuhudia katika mbinu za baadhi ya wanasiasa kutafuta vyeti vya elimu, hatua ya busara ni kuchukulia jambo hilo kwa uzito unaostahili na kutafuta kila mbinu ya kuhakikisha kuna uaminifu.

Kwa sasa, wanasiasa ambao wanafanya juu chini kuficha kisomo chao wanaibua shaka baina ya wananchi na vile vile mbele za wapinzani wao, ilhali vyeti vyao vilikuwa tayari vimeidhinishwa na asasi husika hadi wakakubaliwa na IEBC wawe wagombeaji viti.

Mwananchi anapoamua kujitosa katika siasa za uongozi wa nchi, hafai kutarajia kufurahia uhuru wa kuficha baadhi ya masuala muhimu ambayo yanaweza kuwa msingi wa kudadisi na kutambua uadilifu wake.

Kiongozi bora hafai kuogopa kuweka wazi historia yake kwani hilo litaibua shaka kumhusu.

Uwazi ni mojawapo ya misingi ya uongozi bora ambao unaweza kufanikisha maendeleo ya nchi, na unafaa kuanza kwa mambo ya msingi kama vile kwa mwanasiasa kutoficha historia yake kwa raia.

You can share this post!

Maeneobunge 5 yaliyo na kura nyingi sasa kivutio kwa...

Bodaboda anayedaiwa kuua rafikiye anyakwa na kuzuiliwa

T L