• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
TAHARIRI: Mawaziri wawe mbele kutimiza ahadi za Ruto kwa Wakenya

TAHARIRI: Mawaziri wawe mbele kutimiza ahadi za Ruto kwa Wakenya

NA MHARIRI

HARAKATI ya kuwapiga msasa mawaziri wateule inapoingia siku ya tatu, jambo muhimu zaidi kwa watakaofuzu ni kuhakikisha kuwa maazimio yaliyotolewa na serikali ya Kenya Kwanza wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita, yanapewa uzito zaidi.

Macho hasa yatakuwa kwa sekta za biashara na viwanda, kilimo, leba, elimu, afya, na usalama hasa wa kitaifa.

Sekta ya viwanda na biashara hasa itahitaji weledi wa hali ya juu ikizingatiwa kuwa ndiyo inayotarajiwa na Wakenya wengi kuhakikisha ahadi ya Rais ya kutoa nafasi milioni moja za ajira kwa mwaka inatimizwa.

Sekta hii itakuwa chini ya Bw Moses Kuria iwapo ataidhinishwa na kamati ya bunge inayowapiga msasa mawaziri wateule.

Sekta hii ni muhimu zaidi kwani itasaidia kuwapa ajira vijana wapatao milioni moja ambao hufuzu kila mwaka katika taasisi mbalimbali za elimu.

Ili kuunda nafasi hizo, sharti viwanda zaidi vibuniwe kwa kuwa vilivyopo sasa havitoshi kutoa hata nusu ya fursa za kazi kwa vijana wetu.Hili linaweza kufanikishwa iwapo mazingira ya uwekezaji yataboreshwa hasa kwa wawekezaji wa kigeni.

Aidha, sekta ndogondogo za kilimo ambazo zilidorora kama vile miwa, pamba, mahindi, ngano, majani chai, kahawa na kadhalika zinahitaji kufufuliwa maadamu ndizo zitakazozalisha malighafi ya kutumiwa viwandani.

Rais Ruto, kupitia kwa mawaziri wake husika, anafaa akumbatie kila hatua inayoweza kubuni fursa za kazi hata iwapo zilipendekezwa na washindani wake.

Mpango wa kubuni zoni maalum za kiuchumi jinsi muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya ulivyopendekeza, unaweza kuwanufaisha Wakenya wengi iwapo serikali itaukumbatia.

Sekta ya kilimo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa taifa hili.

Wananchi wanapokuwa na shibe, matatizo mengine mengi hutoweka. Imebainika kuwa mtu aliyeshiba si rahisi awazie kuiba, kwa hivyo visa vya utovu wa usalama. hupungua kwenye shibe.

Naam, Rais ameanza vyema kwa kutoa ruzuku ya mbolea. Lakini atahitajika kutia bidii zaidi kuhakikisha kuwa taifa hili linajitosheleza kwa chakula huku mazao ya ziada yakiuzwa katika mataifa ya kigeni. Elimu, hasa inayompa mwanafunzi maarifa ya kisasa ipewe umuhimu mkubwa.

Mfumo wetu wa elimu uboreshwe ili uweze kuwaandaa wanafunzi kubuni vifaa vya kiteknolojia kuanzia hatua ya kimsingi, jinsi inavyofanyika katika mataifa kama vile Amerika na China.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Ajira: Tutathmini upya taaluma zinazofunzwa...

ZARAA: Waongezea maembe thamani kuvutia soko na faida zaidi

T L