• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 3:25 PM
ZARAA: Waongezea maembe thamani kuvutia soko na faida zaidi

ZARAA: Waongezea maembe thamani kuvutia soko na faida zaidi

NA SAMMY WAWERU

KWA muda mrefu wakulima wa mazao mabichi ya shambani wamekuwa wakikadiria hasara, kupoteza bidhaa hasa zinapofurika sokoni au mawakala kuwahangaisha.

Wanaoathirika zaidi ni wanaolima matunda, mboga na viungo vya mapishi. Kero hiyo imeenea hadi sokoni, wafanyabiashara wasio na njia maalum za kuhifadhi bidhaa zao zikiishia kuharibika na kuoza.

Maembe ni kati ya yanayoongoza, msimu wake yanapokomaa na kuiva yanakuwa katika hatari kuharibika mkulima akikosa wanunuzi.

Kitui ikiwa mojawapo ya kaunti zinazozalisha matunda hayo nchini, wakulima wamepunguziwa kero ya kupoteza mazao kupitia kampuni ya Sun Sweet Fruits ambayo huyaongeza thamani.

Ikiwa eneo la Ithiani, huunda jemu inayotumika badala ya siagi kwenye mkate na mango flakes (vipande vya maembe vilivyokaushwa).

Faith Wanjiru, Meneja wa Mauzo na Soko, anasema kampuni hiyo pia hutengeneza lip balm ambayo ni kama mafuta yanayotumika kulainisha mdomo usikauke kwa kutumia maembe.

Faith Wanjiru, Meneja wa Mauzo na Soko, anasema kampuni hiyo pia hutengeneza lip balm ambayo ni kama mafuta yanayotumika kulainisha mdomo usikauke kwa kutumia maembe. PICHA | SAMMY WAWERU

Jemu inaundwa kwa vipande vya maembe yaliyokaushwa, Wanjiru akidokeza wanapopokea matunda hayo huwa yanapitishwa kwa hatua kadhaa.

“Tunapoyapokea kutoka kwa wakulima, tunayachagua kwa mujibu wa vigezo tulivyoweka,” asema.

Yanayoidhinishwa, huoshwa mara kadha kwa maji safi na klorini kuua viini.

Wanjiru anasema baadaye huwekwa kwenye kreti na kuhifadhiwa katika chumba chenye baridi.

“Yanapopelekwa kiwandani, maganda yanachambuliwa na kuondolewa, kukatwa vipande vipande na kukaushwa kuwa maembe yaliyokaushwa,” aelezea.

Jemu huundwa kwa kutumia maembe yaliyokaushwa huku lip balm ikiundwa kwa kutumia maembe mabichi yaliyokomaa.

Pia wao hutengeneza vijiko kwa kutumia miti na matawi yanayopogolewa.

Ni uvumbuzi wa uongezeaji maembe thamani ambao Sun Sweet Fruits ilitumia kuhamasisha wakulima walioshiriki Maonyesho ya Kimataifa ya Kibiashara na Kilimo Nairobi, mwaka huu 2022.

Maonyesho yaliandaliwa na Muungano wa Kilimo Nchini (ASK), mwenyekiti tawi la Nairobi Joseph Mugo akitaja bunifu na teknolojia za kisasa kuboresha kilimo kama mojawapo ya mbinu kuokoa mazao.

“Wakulima wanahitaji kukumbatia mifumo ya teknolojia za kisasa kuendeleza zaraa na kuongezea mazao thamani ili kuwahi masoko yenye ushindani mkuu,” afisa huyo akahimiza.

Sun Sweet Fruits ilizinduliwa 2019, ambapo ilianza kwa kukausha maembe na kuyauza nje ya nchi, Amerika na Ufaransa.

“Janga la Covid-19 lilipotua Kenya 2020, huduma zilisitishwa kiasi cha kushindwa kuuza mazao ughaibuni. Hatukuwa na budi ila kutafuta njia mbadala kuyaongeza thamani, tukilenga wanunuzi wa ndani kwa ndani,” Wanjiru aambia Akilimali.

Kipimo cha gramu 200 za jemu huuzwa Sh150 bei ya rejareja na jumla, huku gramu 450 Sh250. Vijiko vinaandamana na bidhaa hiyo kama diskaunti kwa wateja.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Mawaziri wawe mbele kutimiza ahadi za Ruto kwa...

UFUGAJI: Mfugaji anayekumbatia kilimo-mseto afurahia...

T L