• Nairobi
  • Last Updated October 1st, 2023 9:40 PM
TAHARIRI: Panayo haja ya Rais Ruto kuunganisha Wakenya wote

TAHARIRI: Panayo haja ya Rais Ruto kuunganisha Wakenya wote

NA MHARIRI

UCHAGUZI mkuu wa Agosti 9 ulikuwa wa kipekee kwa jinsi ulivyokuwa na ushindani mkali kuliko mwingineo wowote ambao umewahi kufanyika nchini.

Mshindi, ambaye ni Rais William Ruto, alizoa takribani kura milioni 7.1 huku mshindani wake mkuu, Bw Raila Odinga akizoa milioni 6.9.

Mshindi alimpita nambari mbili kwa kura takribani 200,000 pekee.

Kwa kuzingatia matokeo hayo, taifa hili liligawika katikati ambapo idadi inayomuunga Rais mkono ni sawa na ile isiyomuunga.

Ukichunguza, unagundua kuwa baadhi ya wafuasi wa waziri mkuu wa zamani, Bw Raila Odinga, wangali na machungu mioyoni wala hawajapata uthabiti katika dhamiri zao kushinda ushinde huo katika kura na kampeni kali zenye chuki.

Hatua hii inamhitaji Rais Ruto, ambaye ndiye ishara ya umoja nchini, kuanza kutumia mbinu zote awezazo kuhakikisha kuwa kuna uwiano, mapatano na umoja miongoni mwa Wakenya.

Mojawapo ya mikakati inayoweza kutumika kuleta uwiano wa kweli ni kuhakikisha kuwa serikali inazindua miradi katika kila eneo, iwe eneo hilo lilimpigia Dkt Ruto kura au la.

Pili ni Rais na wabunge wa mrengo wake kujizatiti kuepuka matamshi yoyote yanayoibua hisia za kampeni na ushindani.

Katika siku ya Jamhuri Dei, Rais alitoa ahadi nyingine inayoweza kuwaleta pamoja Wakenya; kinyang’anyiro cha soka cha Bottom-Up ambacho kitachezwa katika kaunti zote na kisha upeo wake kuishia kwenye fainali za kitaifa.

Kwa kutoa ahadi hiyo, Rais ‘ataua’ ndege wawili kwa jiwe moja. Mbali na dimba hilo kuchochea ukuaji na utambuaji wa vipawa katika ngazi za mashinani, litasaidia kuleta utangamano na mtagusano baina ya makabila na matabaka mbalimbali ya Wakenya.

Michezo imebainika kuwa wenzo aula wa kupambana na uhasama wa kikabila aina nyinginezo za chuki na hiana.

Hatua nyingine ambayo Rais amependekeza inayofaa kuungwa mkono kwa kuwa itapunguza uhasama uliopo, ni kuunda afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani.

Hata hivyo, itakuwa bora afisi hiyo ibuniwe kwa kufuata sheria ili isije ikaharamishwa na mahakama jinsi ilivyofanyika kwa mpango wa mapatano wa BBI.

Taifa linapokuwa na umoja, ustawi hupatikana kwa haraka maadamu hasira za mioyoni hupungua na kuruhusu ari na ghera ya kufanya kazi vyema kujidhihirisha.

Haya yote yana maana kuwa Rais achukue hatua zozote awezazo kukuza umoja, mapatano na utangamano wa kitaifa.

You can share this post!

Infantino na FIFA waridhika kwamba michuano ya Kombe la...

Korti yaagiza hoteli kulipa mfanyakazi aliyeachishwa kazi...

T L