• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 2:32 PM
Infantino na FIFA waridhika kwamba michuano ya Kombe la Dunia imetia fora nchini Qatar

Infantino na FIFA waridhika kwamba michuano ya Kombe la Dunia imetia fora nchini Qatar

NA JOHN ASHIHUNDU

RAIS wa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa) Gianni Infantino amesema fainali za Kombe la Dunia za Qatar 2022 ndizo bora zaidi kuwahi kuandaliwa tangu mashindano hayo yafanyike kwa mara ya kwanza nchini Uruguay mnamo 1930.

Alisema ufanisi huo umeondoa dhana kwamba mataifa madogo kama Qatar hayana uwezo wa kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa.

Mashindano hayo ya Makala ya 22 yalileta pamoja timu 32 zilizoshindana tangu Novemba 20, ambapo fainali yake ni Jumapili kati ya mabingwa watetezi Ufaransa dhidi ya mabingwa mara mbili, Argentina.

Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa michuano hiyo kufanyika katika eneo la Mashariki ya Kati na ardhi ya Uarabuni kwa mara ya kwanza.

“Fifa kwa jumla imepongeza fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu, pamoja na watu wote waliohusika kuzifanikisha,” Infantino alisema katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Doha Ijumaa.

Kiongozi huyo wa Fifa alisema kadhalika baraza hilo limekubali kuidhinisha baadhi ya mapendekezo, ikiwa pamoja na kupandisha bajeti ya fainali zijazo zitakazofanyika baada ya miaka mine.

Infantino alisema bajeti ya msimu wa 2023-2026 itagharamiwa kwa bajeti ya Sh923 bilioni, kutoka kwa 787 bilioni zilizotumika msimu wa 2018-2022.

Fifa kawaida hutoa msaada wa kifedha kwa mashirika wanachama wake. Kwa mfano Kenya ilipokea ufadhili wa Sh120 milioni, kulingana na taarifa ya matumizi ya kifedha iliyotolewa na shirikisho hilo la kimataifa.

“Tayari baraza la Fifa limepitisha bajeti ya Sh1.35 bilioni kutumika kwa miaka mine ijayo, ambapo Sh246 bilioni zitatumika kuimarisha vipaji chini ya aliyekuwa kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, ambaye ni Mkuu wa Kimataifa wa kuimarisha vipaji katika kitengo cha shirikisho hilo.

Fifa ilieleza mpango huo wa 2023-2026 kuwa mkubwa zaidi kuwahi kufanyika, ambao madhumuni yake ni kusaidia mashirika yake kufikia upeo wa juu kimataifa.

Alisema, mashindano ya wanasoka wasiozidi umri wa miaka 17 kwa timu za wavulana na wasichana yatafanyika kila mwaka, ambapo idadi ya timu zitakazoshirki itaongezeka kutoka 24 kwa timu za wavulana na 16 za wasichana. Mechi za Kombe la Klabu Bingwa zitafanyika nchini Morocco mwezi Februari 2023.

Infantino alisema nchini Qatar, mechi moja imekuwa ikivutia mashabiki 52,760, wakati idadi ya juu zaidi ikifikia 88,666 wakati wa mechi ya Kundi C kati ya Argentina na Mexco iliyochezewa Lusail Stadium. Kufikia sasa, mashabiki wapatao 3.7 milioni wamehudhuria mechi 62 zilizochezwa.

Kesho, Jumamosi, Morocco watakutana na Croatia kutafuta nafasi ya tatu na nne kwenye mechi itakayochezewa Khalifa International Stadium kabla ya fainali ya Jumapili kati ya Argentina na Ufaransa.

  • Tags

You can share this post!

Gavana wa Lamu awapa mawaziri kandarasi za miaka 2

TAHARIRI: Panayo haja ya Rais Ruto kuunganisha Wakenya wote

T L