• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 12:25 PM
TAHARIRI: Polisi waangalie usalama wa raia kwenye mikutano ya kampeni

TAHARIRI: Polisi waangalie usalama wa raia kwenye mikutano ya kampeni

NA MHARIRI

KUFUNGULIWA rasmi kwa kampeni mnamo Mei 29 kulitoa fursa kwa waniaji nyadhifa za uongozi kuuza sera zao kwa wapigakura.

Kampeni hizo ni muhimu kwa kuwa zinawapa wananchi nafasi ya kusikia sera za wanaotaka kuchaguliwa. Kwenye kampeni, serikali imekuwa ikiweka ulinzi lakini ni kama maafisa hao wanajushughulisha na mambo tofauti kabisa.

Wiki hii tu kumeshuhudiwa matukio matatu yanayozua maswali kuhusu kazi ya polisi kwenye mikutano ya siasa.

Kisa cha kwanza kilitokea katika soko la Nyaramba, Borabu kaunti ya Nyamira. Mbunge wa eneo hilo, Bw Ben Momanyi alipokuwa akihutubu, video iliyosambazwa mitandaoni inaonyesha Bw Momanyi kutoshtuka gari lilipopita kwenye umati na kujeruhi mtu. Yeye alionekana kutazama mara moja na kuwataka wakazi waendelee kusikiliza hotuba yake.

Licha ya watu kusikika wakipiga kelele kumweleza gari lilikuwa limeingia kwenye umati na mtu mmoja alikuwa amepata majeraha, mbunge huyo anaonekana kutojali.

Katika kaunti ya Meru, mtu na mkewe walikufa kati ya Nkubu na Chogoria, pikipiki yao ilipogongana na lori la msafara wa kampeni.

Lori husika lilikuwa likibeba wafuasi wa mgombeaji wa kiti cha eneobunge la Imenti Kusini, Dkt Shadrack Mwiti wa chama cha Jubilee.

Na kisa cha mwisho kilihusisha mbunge wa Garissa Mjini, Bw Aden Duale, ambaye kwenye mojawapo ya kampeni za chama cha United Democratic Alliance (UDA) nusura avuliwe nguo. Bw Duale aliyekuwa akihutubu, ni kama alimkasirisha mmoja wa waliokuwa kwenye mkutano. Bila kufikiri zaidi, jamaa alionekana kumkabili Bw Duale na kujaribu kumvua suruali.

Matukio ya Kisii na alikokuwa Bw Duale, yalijiri mbele ya macho ya maafisa wa polisi waliokuwa kwenye mikutano hiyo ya kisiasa. Kufikia sasa, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na polisi kueleza ni hatua gani walizochukua dhidi ya waliosababisha ajali, ama huyo jamaa aliyetaka kumshambulia Bw Duale.

Jukumu la polisi, hata wakati usipokuwa wa kampeni, ni kulinda mali na maisha ya wananchi. Maisha ya raia yanapotishiwa na dereva anayeendesha gari ndani ya umati, hata kama gari hilo limeharibika breki, ni ya maana. Dereva husika ilifaa akamatwe na kuandikisha taarifa katika kituo cha polisi. Magari yanayotumika kwenye shughuli za kampeni yafaa yawe katika hali nzuri. Yasiwe yakibeba watu kupita kiasi ilhali hayana bima, magurudumu yameisha au breki hazijakazwa vizuri.

Wizara ya Usalama wa Ndani iwape maagizo maalumu maafisa wa polisi wanaotumwa kwenye mikutano ya kampeni, kwamba jukumu lao ka kwanza ni usalama wa wananchi.

  • Tags

You can share this post!

Wanandoa wafariki baada ya kurudiana

Wanawake wajitosa siasa za ngazi ya juu

T L