• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 6:50 AM
Wanawake wajitosa siasa za ngazi ya juu

Wanawake wajitosa siasa za ngazi ya juu

NA CHARLES WASONGA

HISTORIA imeandikishwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu baada ya idadi kubwa ya wanawake kuidhinishwa kuwania nyadhifa za juu.

Baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kukamilisha shughuli ya kuwaidhinisha wagombeaji mnamo Jumanne wiki hii, imeibuka wanawake watatu watashiriki uchaguzi wa urais kama wagombea wenza huku 16 wakiidhinishwa kugombea ugavana.

Hii ina maana kuwa kati ya wagombea urais watatu walioidhinishwa na IEBC, ni Naibu Rais William Ruto pekee ambaye mgombea mwenza wake ni mwanaume, Rigathi Gachagua.

Wanawake walioidhinishwa kuwa wenza wa wagombea urais ni Kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua ambaye anashirikiana na mgombea urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga, Justina Wambui akiwa na George Wajackoya wa Chama cha Roots na Ruth Mutua ambaye ni mgombea mwenza wa David Mwaure Waihiga wa chama cha Agano.

WALIOIDHINISHWA

Wanawake 16 kati ya 23 waliotuma maombi ya kuwania ugavana nao watakuwa debeni Agosti 9 baada ya kupata kibali kutoka IEBC. Hao ni pamoja na Fatma Achani (Kwale), Susan Kihika (Nakuru), Aisha Jumwa (Kilifi), Gladys Wanga (Homa Bay), Cecily Mbarire (Embu) na Wangui Ngirici (Kirinyaga).

Charity Ngilu (Kitui) na Anne Waiguru (Kirinyaga) wanatetea viti vyao kwa awamu ya pili, wakiwa ndio wanawake pekee pamoja na marehemu Joyce Laboso wa Bomet walioshinda ugavana kwenye uchaguzi mkuu wa 2017.

Wanawake wengine walioidhinishwa kuwania ugavana mwaka huu ni Patience Nyange (Taita Taveta), Profesa Agnes Mwagombe (Taita Taveta), Millicent Oduor (Siaya), Mwende Gatabaki (Kiambu), Rose Mulwa (Machakos), Esther Waringa (Nairobi) na Agnes Kagure (Nairobi).

Wanawake zaidi pia wameteuliwa kuwa wagombea wenza wa ugavana wakiwemo Joyce Kiprop (Nakuru) na Priscilla Mwangeka (Taita Taveta).

USENETA

Kiti cha useneta pia kimevutia wanawake kadha wakiwemo Profesa Margaret Kamar (Uasin Gichu), Priscilla Nyokabi (Nyeri), Lilian Mbogo Omollo (Embu), Tabitha Karanja (Nakuru), Margaret Masiko (Mombasa), Joyce Rita (Mombasa), Anne Njambi (Taita Taveta) na Hellen Kigai (Murang’a).

Wanaharakati wa haki za wanawake na wachanganuzi wa masuala ya kisiasa wanasema idadi kubwa ya wanawake waliodhinishwa kuwania nyadhifa za juu katika uchaguzi wa Agosti 9 ni matunda ya juhudi za miaka mingi ya kutetea usawa wa kijinsia.

“Huu ni mwamko mpya katika uongozi wa wanawake tangu taifa hili lilipopata uhuru. Japo wanawake wengi wamewania urais na kufeli, mwaka huu kuna matumaini makubwa wa mwanamke kushikilia wadhifa wa naibu rais,” mkereketwa wa haki za wanawake na uongozi bora Daisy Amdanyi akaambia Taifa Leo.

HISTORIA

Akihutubu katika bustani ya Uhuru Gardens wakati wa Madaraka Dei, Rais Uhuru Kenyatta alirejelea suala hilo alipokuwa akielezea hatua ambazo serikali yake imepiga katika kutoa nafasi za uongozi kwa wanawake: “Ikiwa itakuwa mapenzi ya Wakenya, kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hili mwanamke atashikilia nafasi kuu katika asasi ya urais.”

Kwa upande wake, aliyekuwa Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nyeri, Priscilla Nyokabi, ambaye mwaka huu anawania kiti cha seneta wa kaunti hiyo, ameelezea matumaini kuwa idadi kubwa ya wanawake watashinda viti katika uchaguzi wa mwaka huu.

“Katika uchaguzi mkuu wa 2013 hakuna mwanamke aliyeshinda ugavana lakini 2017 kwa mara ya kwanza Kenya ilipata magavana watatu wa kike. Mwaka huu kuna matumaini makubwa ya idadi hiyo kuongezeka,” akaeleza Bi Nyokabi.

Katika viti vingine vinavyowaniwa ikiwemo ubunge na uwakilishi wadi, idadi kubwa ya wanawake wamejitosa ulingoni kukabiliana na wanaume.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Polisi waangalie usalama wa raia kwenye mikutano...

VALENTINE OBARA: Mahakama zisishike mateka uchaguzi wa...

T L