• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
TAHARIRI: Viongozi waache kuingiza siasa katika mambo yahusuyo sheria

TAHARIRI: Viongozi waache kuingiza siasa katika mambo yahusuyo sheria

NA MHARIRI

MADAI yanayotolewa na wanasiasa kuhusu utumizi mbaya wa raslimali za umma ni ya kushangaza sana.

Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula na Kinara wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi wamejitokeza kumtetea mbunge wa Kimilili, Didmus Barasa, anayetuhumiwa kutumia gari la serikali katika kampeni zake.

Tuhuma hasa ni kuwa, Bw Barasa, aliamua kuligeuza gari hilo linalotumika katika afisi za NG-CDF, kuwa mali yake binafsi, na kulipaka rangi za chama cha UDA pamoja na kuweka picha yake na ile ya Naibu Rais William Ruto.

Polisi wanasema alibadili nambari za usajili GK948J na kuweka za kibinafsi, ilhali yeye si afisa wa Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA) wala afisa wa polisi anayehusika na masuala ya trafiki.

Bw Wetang’ula ambaye ni wakili anayeheshimika, aliamua kuingiza siasa katika suala la kisheria, na kumtetea Bw Barasa kuwa anachimbwa na serikali kwa kuwa hayuko kwenye muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Kudai kuwa Bw Barasa si wa kwanza kutumia gari la serikali kwenye kampeni, ni kutaka umma ushawishike kuwa hakuna ubaya wowote kwa mtu kugeuza gari la serikali kuwa la kibinafsi.

Sheria ya nchi ni kuwa, hata kama gari lilikuwa la serikali, linapobadilishwa kuwa la raia, nambari yake ya awali hubaki, isipokuwa mwanzo kunakuwa na neno EX. Kwa mfano hilo gari lingekuwa Ex GK948J.

Viongozi hao wanadai kuwa hata Kinara wa ODM Raila Odinga anatumia magari ya serikali yenye nambari za usajili wanazodai kuwa KCY.

Swali ni je, Bw Odinga alibadili nambari hizo za magari kutoka GK?

Pili, amewahi kuyapaka magari hayo rangi za kampeni?

Ukweli ni kuwa Bw Odinga, Bw Mudavadi na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka pamoja na aliyekuwa Makamu wa Rais Moody Awori wanatumia magari ya serikali kutokana na nyadhifa walizowahi kushikilia awali.

Je, Bw Mudavadi mwenyewe amewahi kupaka magari ya serikali rangi ya chama chake cha ANC? Ashawahi kuondoa nambari za usajili za serikali na kuweka ya kiraia?

Hata kama wanasiasa wanasema huu ni muda wa kampeni, ni muhimu kutofautisha siasa na sheria. Alichofanya Bw Barasa ni makosa na lazima awajibikie makosa yake. Serikali iwachukulie hatua wote wanaotumia vibaya mali ya wananchi, bila kujali wako katika mrengo gani wa kisiasa.

You can share this post!

Redio za lugha mama zatakiwa ziwe na vipindi kuhusu jamii

Musalia, Wetang’ula wamtetea Didmus

T L