• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 6:30 PM
VALENTINE OBARA: Mahakama zisishike mateka uchaguzi wa ugavana Mombasa kupitia maamuzi tata

VALENTINE OBARA: Mahakama zisishike mateka uchaguzi wa ugavana Mombasa kupitia maamuzi tata

NA VALENTINE OBARA

UAMUZI wa aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, kutaka kuwania ugavana Mombasa kwenye uchaguzi wa Agosti unazidi kuibua mjadala mkali miongoni mwa wananchi.

Huku kesi nyingi iwapo anastahili kukubaliwa kuwania zikiendelea kusikilizwa mahakamani, wataalamu wa kisheria pia wamegawanyika pande mbili kuhusu hatima yake.

Ni wajibu wa mahakama kuhakikisha kesi zote zinazohusu suala hili zimekamilishwa haraka iwezekanavyo.

Hii ni kwa sababu, kuna hatari ya kuvuruga mipango ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuandaa uchaguzi wa ugavana Mombasa endapo hizi kesi zitaendelea kujikokota mahakamani.

Hatungependa kutokee hali ambapo kuchelewa kwa maamuzi kunaweza kufanya IEBC ishurutishwe kumjumuisha Bw Sonko miongoni mwa wawaniaji kisha baadaye igundulike hatua hiyo ilikiuka sheria.

Vilevile, itakuwa hasara kubwa iwapo tume hiyo chini ya Mwenyekiti Wafula Chebukati, italazimishwa kumwacha nje kisha baada ya uchaguzi kukamilika isemekane alikosewa haki zake za kikatiba.

Isitoshe, hatuwezi pia kupuuza uwezekano wa mtu kwenda mahakamani kutaka uchaguzi wa ugavana usiandaliwe Mombasa hadi uamuzi wa mwisho kumhusu Bw Sonko utolewe. Hii ni kwa sababu mahakama zetu zimefahamika kutoa maamuzi ya kiajabu ajabu tangu Katiba ifanyiwe marekebisho mnamo 2010.

Bw Sonko anakumbwa na vikwazo tele kwa kuwa, alibanduliwa mamlakani Nairobi baada ya bunge la kaunti hiyo na seneti kumpata na hatia za ukiukaji wa maadili.

Ingawa kuna viongozi wengine ambao pia walibanduliwa kwa misingi hiyo, akiwemo aliyekuwa gavana wa Kiambu, Bw Ferdinand Waititu, usisitizaji wa Sonko kuwa debeni Mombasa umemfanya awe gumzo zaidi kuhusu suala la ikiwa waliotimuliwa wanafaa kukubaliwa kuwania tena.

Msimamo wake ni kuwa, hafai kuzuiwa kwa sababu bado kuna kesi alizowasilisha mahakamani akitaka uamuzi wa bunge la kaunti na seneti kumfurusha kwa sababu ya kukiuka maadili ubatilishwe.

Hata hivyo, kilicho wazi kwa sasa ni kuwa, sheria haruhusu Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumwidhinisha mtu aliyeng’atuliwa mamlakani kwa ukiukaji wa sheria kuwania kiti chochote kingine cha kisiasa isipokuwa uamuzi huo ubatilishwe. Maamuzi kumhusu Bw Sonko kuelekea kwa uchaguzi wa Agosti bila shaka yatakuwa na uzito mkubwa ambao utaathiri siasa, hasa za serikali za kaunti, kwa miaka ya usoni.

Katika miaka iliyopita, magavana walikuwa wakilalamika kuwa madiwani wa kaunti zao hutishia kuwatimua iwapo hawatawatekelezea matakwa yao kama vile kuwaongezea mgao wa fedha za marupurupu katika bajeti za matumizi ya pesa za umma.

  • Tags

You can share this post!

Wanawake wajitosa siasa za ngazi ya juu

KINYUA BIN KING’ORI: Wawaniaji urais wathibitishe...

T L