• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:55 AM
WANDERI KAMAU: Mvutano wa Mahakama, Afisi ya Rais hatari kwa nchi

WANDERI KAMAU: Mvutano wa Mahakama, Afisi ya Rais hatari kwa nchi

Na WANDERI KAMAU

KULINGANA na historia, mfumo wa utawala wa kisiasa duniani ulianza mwaka 2300 BCE (Kabla ya Ujio wa Kristo), katika falme ya Mesopotamia, ambayo kwa sasa ni nchi ya Iraq.

Ni mfumo ulioshirikisha uwepo wa nguzo tatu kuu—Bunge, Idara ya Mahakama na Afisi ya Rais, Waziri Mkuu au Mfalme, kulingana na aina ya utawala unaozingatiwa na nchi ama jamii husika.

Kimsingi, matawi hayo matatu huwa yanategemeana ili kukamilisha mchakato mzima wa utawala.

Jukumu kuu la Bunge huwa ni kutunga sheria, Idara ya Mahakama huwa ni kufasiri sheria hizo, huku Afisi ya Rais ikitwikwa jukumu la kutekeleza sheria hizo.

Hata hivyo, Katiba ya nchi husika inamhitaji kila mwanajamii kuzingatia sheria zilizopo bila kujali hadhi yake katika jamii hiyo.

Vile vile, ni muhimu kwa matawi hayo matatu kuendesha utendakazi wao kwa kujali athari za vitendo vyake kwa matawi mengine au mustakabali wa nchi husika kwa ujumla.

Sababu ya urejeleo huu ni mvutano ambao umekuwa ukionekana kuwepo kati ya Afisi ya Rais na Idara ya Mahakama.

Mvutano huo umekuwa ukidhihirika wazi kwenye baadhi ya maamuzi tata ambayo yamekuwa yakitolewa na mahakama zetu.

Ni maamuzi ambayo yamekuwa yakizua maswali, kuhusu athari zake kwa jamii ikiwa yangetekelezwa kama vile mahakama zilivyoagiza.

Ingawa Idara ya Mahakama nchini ilijizolea sifa nyingi kote duniani 2017 baada ya Mahakama ya Juu kufutilia mbali uchaguzi mkuu wa urais, uhusiano wake na matawi mengine serikalini ulianza kudorora.

Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga alianza kulalamika idara hiyo “kuhangaishwa” na asasi nyingine serikalini, hasa Afisi ya Rais.

Kwanza, alilalamikia kupunguzwa kwa bajeti yake, kuhangaishwa kwa baadhi ya majaji kwa kile kilionekana kama vitisho kutokana na maamuzi ya kesi zilizowasilishwa kwao.

Pia alilalamikia “kukosewa heshima” kwenye hafla muhimu nchini, kwa kutowekewa zulia jekundu kama maafisa wengine wa serikali.

Licha ya malalamishi hayo, Rais Uhuru Kenyatta alionekana kutozingatia rai na vilio vya Jaji Maraga.

Katika siku za hivi karibuni, mahakama zimekuwa zikitoa maamuzi ambayo yanapinga ama kukosoa karibu kila zoezi linaloendeshwa na serikali.

Ni maamuzi ambayo Rais Kenyatta ameyakosoa hadharani, akieleza kutoridhishwa nayo.

Mfano ni uamuzi wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa kuharamisha Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI).

Kwenye hotuba zake, amekuwa akitaja uamuzi huo kama “kosa la kisheria”, akishikilia kuwa katika siku zijazo, mpango huo utafufuliwa upya.

Wengi walitarajia taswira iliyopo ingepungua baada ya Jaji Mkuu, Bi Martha Koome, kuchukua usukani, lakini hali imebaki hivyo.

Uchaguzi mkuu wa 2022 unapoendelea kukaribia, ni lazima matawi hayo mawili yatathmini upya uhusiano wake ili kutoiingiza nchi katika giza la kiutawala kama vile hali ilivyokuwa 2007.

Lazima yafahamu utendakazi wake unawaathiri mamilioni ya Wakenya.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mlipuko wa trela la mafuta waua 77 Haiti

JUMA NAMLOLA: Serikali iboreshe uchukuzi wa umma kuokoa...

T L