• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 2:11 PM
WANDERI KAMAU: Tubadilishe taratibu za kuwachagua magavana

WANDERI KAMAU: Tubadilishe taratibu za kuwachagua magavana

Na WANDERI KAMAU

UCHAGUZI mkuu wa Agosti unapokaribia, pengine huu ni wakati mwafaka zaidi kwa Wakenya kutathmini umuhimu wa baadhi ya nyadhifa za kisiasa zilizopo na ikiwa zinachangia maendeleo ya nchi kwa namna yoyote ile.

Kufikia sasa, ni miaka tisa tangu mfumo wa ugatuzi kuanza kutekelezwa nchini baada ya serikali ya Jubilee kuchukua uongozi mnamo 2013.

Kwa muda huo wote, nafasi ambayo imeibukia kuwa muhimu zaidi ni ile ya ugavana.

Ni nafasi ambayo imedhihirisha kuwa kaunti huendelea au hubaki nyuma kimaendeleo kulingana na gavana aliyechaguliwa na wenyeji.

Kimsingi, gavana ni kama ‘mzazi’ wa wenyeji wa kaunti husika. Hili ni kutokana na mamlaka aliyo nayo, kiwango cha fedha anachotengewa na ushawishi wa kisiasa alio nao. Tangu 2013, kaunti ambazo zimefanikiwa kuwachagua magavana wazuri, wachapa kazi na wasio wafisadi zimefurahia matunda ya ugatuzi.

Vivyo hivyo, kaunti ambazo ziliwachagua magavana kwa misingi ya hisia, wimbi la kisiasa lililopo, uwezo wake wa kifedha au misukumo tofauti ya kisiasa bila kuzingatia aina ya utendakazi wake zimejutia maamuzi yao.

Umuhimu wa nafasi ya ugavana umeibua maswali kuhusu ikiwa inapaswa kuwa ya kisiasa.

Ni maswali ambayo yameibuliwa na watu binafsi kama wasomi wa sayansi ya siasa, wataalamu wa sheria, wataalamu wa masuala ya utawala, wanahistoria, wanaharakati wa haki za umma kati ya wengine. Vile vile, taasisi tofauti zimejitokeza kuirai Kenya kutathmini upya ikiwa nafasi ya ugavana inapaswa kuwa ya kisiasa.

Kulingana na wataalamu walioshiriki kwenye zoezi la kuandika Katiba ya 2010, walitoa baadhi ya mifumo ya kiutawala na kisiasa inayotumika kwa sasa kutoka kwa katiba za nchi kama Uingereza, Amerika na Canada.

Hili ni ikizingatiwa kuwa hata chini ya Katiba ya Zamani (1963), Kenya bado ilikuwa ikiiga Uingereza kwenye mfumo wake wa utawala.

Ingawa kupitishwa kwa Katiba ya nchi hakumaanishi haipaswi kutathminiwa upya, kuna haja kubwa Kenya kubadilisha mfumo wa kuwachagua magavana.

Pili, hili halipaswi kuoanishwa na maamuzi ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa kuharamisha Mpango wa Kubadilisha Katiba (BBI), uliopigiwa debe na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.

Hata hivyo, pendekezo hili linapaswa kuonekana kama njia ya kuboresha kiwango cha magavana tunaowachagua.

Katika nchi nyingi za Jumuiya ya Madola (ikiwemo Uingereza), magavana huwa hawachaguliwi moja kwa moja na raia.

Badala yake, huwa wanachaguliwa na baraza maalum la wawakilishi katika majimbo wanayoyawawakilisha.

Mabaraza hayo huwajumuisha watu wanaowakilisha sekta mbalimbali katika jamii, ili kuhakikisha kila mmoja amewakilishwa kwenye mchakato huo.

Nchini Canada, utaratibu wa kuwachagua magavana ni uo huo.

Nchini Amerika, hali huwa tofauti kwani wao huchaguliwa na raia, japo ni baada ya taratibu kali za kuwateua wawaniaji zinazoendeshwa na vyama kama Democratic na Republican.

Ni kutokana na hayo ambapo ni vigumu kumsikia gavana anayeondolewa mamlakani au aliyefunguliwa mashtaka ya ufisadi katika nchi hizo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo, Gideon sasa njia panda kisiasa baada ya OKA...

WANTO WARUI: Tofauti baina ya walimu na mwajiri wao...

T L