• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:53 AM
WANTO WARUI: Tofauti baina ya walimu na mwajiri wao zisivurugie maisha watahiniwa

WANTO WARUI: Tofauti baina ya walimu na mwajiri wao zisivurugie maisha watahiniwa

NA WANTO WARUI

CHAMA cha walimu wa shule za sekondari (KUPPET) kimetoa tishio la mgomo wakati wa mtihani wa kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) unaotarajiwa kufanywa katika mwezi wa Machi-Aprili mwaka huu wa 2022.

KUPPET imesema kuwa ikiwa mishahara yao haitaongezwa kwa asilimia sabini (70%), basi walimu wataweka majembe yao chini bila kujali kama mitihani itakuwa ikiendelea.

Kulingana na KUPPET, mkataba kuhusu nyongeza hii ya mishahara ushatiwa saini baada ya makubaliano lakini hakuna chochote kilichotekelezwa na mwajiri wa walimu (TSC) kufikia sasa.

KUPPET imesema kuwa haitaki kuitwa tena katika mkutano wa majadiliano bali inataka nyongeza hii ya mishahara itekelezwe mara moja.

Kwa siku nyingi, mvutano kati ya walimu na mwajiri wao kuhusu nyongeza za mishahara umedhalilisha masomo wakati mwingine migomo ikichukua muda mrefu mno. Katika nyakati kama hizi, wanafunzi na wazazi ndio huumia huku wakingojea suluhisho kutoka kwa serikali. Licha ya walimu kuwa katika migomo na kuendeleza shughuli nyinginezo za kiuchumi nyumbani, huwa wanadai malipo kamili ya mishahara yao kwa kipindi chote hicho wanapokuwa wamegoma.

Ingawa ni haki ya walimu kudai malipo yanayolingana na kazi wanayofanya, ni makosa kuathiri masomo ya wanafunzi wasio na hatia na ambao wanajijengea msingi bora wa maisha yao. Wanafunzi hao pia wana haki ya kupata elimu bila usumbufu wowote. Tofauti baina ya walimu na mwajiri wao, TSC, hazifai kuathiri masomo kamwe.

Aidha, serikali ina jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa wanafunzi wote nchini wanapata elimu bora. Katika taifa linaloongoza kiuchumi na kimaendeleo Afrika Mashariki na kati, sekta ya elimu ipewe umuhimu unaostahili.

ni muhimu sana kwani ndio msingi wa kuiwezesha nchi kusonga mbele zaidi. Wizara ya Elimu inafaa kuhakikisha kuwa mkataba wowote kuhusu mshahara unaowekwa saini na walimu na TSC umeheshimiwa na kufuatwa bila pingamizi zozote.

Ni muhimu pia kufahamikiwa kuwa wanafunzi wanaosubiri kufanya mtihani wao wa KCSE wamepitia katika dhiki nyingi. Kutokana na kukatizwa kwa masomo kwa sababu ya mkurupuko wa ugonjwa wa Covid-19 pamoja na mtafaruku ambao umekuwa shuleni wa migomo ya wanafunzi, hapana shaka wanafunzi wamepoteza sana. Walimu wamepitia kazi ngumu wakijaribu jinsi ya kuwainua wanafunzi hawa.

Basi ni kinaya kikubwa kwa walimu wale wale waliokuwa wakidai kuwa hawana muda wa kutayarisha wanafunzi vyema kusema kuwa sasa wanataka kugoma. Kuna njia mbadala za kutatua tatizo kama hili pasipo kuathiri wanafunzi ambao wamengojea mtihani wao kwa hamu kubwa.

Viongozi wa chama cha walimu wa sekondari (KUPPET) waweke madai yao kando na kuwafikiria kwanza wanafunzi wanaowafunza.

  • Tags

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Tubadilishe taratibu za kuwachagua magavana

TAHARIRI: Bodi iziondoe dawa hatari hospitalini

T L