• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 2:31 PM
WANDERI KAMAU: Usahaulifu: Gonjwa hatari sana wanalougua Wakenya

WANDERI KAMAU: Usahaulifu: Gonjwa hatari sana wanalougua Wakenya

Na WANDERI KAMAU

KENYA ni jamii ya kipekee sana duniani.

Pengine Wakenya ndio watu pekee wanaofanya makosa kimakusudi na baadaye kuanza kulalamikia makosa yao wenyewe.

Makosa hayo yanafanyika katika kila nyanja—kisiasa, kiuchumi, kielimu, kidini na kitamaduni.Kisiasa, Wakenya huwachagua wawakilishi wao kwa hisia, mihemko na misukumo ya kisiasa iliyopo, hivyo kukosa kutathmini uwezo wao kwa undani.

Wakenya hukubali kudanganywa na wanasiasa kuwa “fulani” ni hasimu wake, bila kusaka ukweli wa kauli za mwanasiasa husika.Kwa mfano, kuna kundi linaloamini kuwa Naibu Rais William Ruto ni adui mkubwa wa Rais Uhuru Kenyatta, baada ya wawili hao kutofautiana kisiasa.

Hali ilivyo sasa, wanaamini kuwa kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, ndiye rafiki halisi wa Rais Kenyatta, hasa baada yao kuungana kupitia handisheki mnamo Machi 9, 2018.

Hata hivyo, Wakenya husahau kuwa kwa muda mrefu, Rais Kenyatta na Bw Odinga wamekuwa washindani wakali wa kisiasa, waliorushiana cheche kali za matusi hata yasiyoandikika.

Kwenye refarenda ya 2005, Rais Kenyatta alikuwa kwenye kambi moja na Bw Odinga iliyopinga Rasimu Mpya ya Katiba iliyokuwa ikipigiwa debe na Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Miaka miwili baadaye—kwenye uchaguzi mkuu wa 2007—Rais Kenyatta alikuwa kwenye kambi moja na Bw Kibaki, kupinga azma ya Bw Odinga kuwania urais.

Kwenye chaguzi kuu za 2013 na 2017, wawili hao (Rais Kenyatta na Bw Odinga) walikuwa kwenye kambi tofauti za kisiasa.

Wawili hao sasa wanajifanya kuwa marafiki: je, ni nani atakayewaamini wanasiasa hao ikizingatiwa awali walikuwa ‘mahasimu’ wa kisiasa

Taswira iyo hiyo ndiyo inayowaandama Rais Kenyatta na Dkt Ruto.

Mwaka 2002, walikuwa pamoja katika chama cha Kanu.

Mwaka 2007, Dkt Ruto alikuwa kwenye kundi la ‘Pentagon’ lililomuunga mkono Bw Odinga kuwania urais, huku Rais Kenyatta akiwa miongoni mwa viongozi waliompigia debe Rais Kibaki.

Wawili hao walikuwa pamoja kwenye chaguzi kuu za 2013 na 2017, japo “wakakosana” mwanzoni mwa 2018.

Maswali ambayo Wakenya wanapaswa kujiuliza ni: Mbona Rais Kenyatta na Dkt Ruto “wamekosana” tu baada ya muda wa Rais kuelekea tamati? Ni ipi ndiyo sababu fiche ya ‘kukosana’ kwao”? Mbona wakati huu ndio wamegeukiana na kuwa “maadui”?

Mbali na siasa, si mara moja utasikia vifo vya Wakenya walioangamia kutokana na mikasa kama unywaji pombe haramu au kuchota mafuta kwenye trela iliyoanguka.

Kwa mfano, Agosti 2021, watu watano walifariki katika kijiji cha Hodihodi, eneo la Bahati, Kaunti ya Nakuru, baada ya kudaiwa kunywa pombe haramu.

Miezi minne baadaye (Desemba), watu wengine watano walifariki katika kijiji cha Jawatho, Njoro, kaunti iyo hiyo, baada ya kunywa pombe haramu pia.

Hata ingawa visa vingi vinatajwa kuchangiwa na umaskini, je waathiriwa hao hawakujifunza kutokana na wenzao waliofariki Agosti?

Ukweli ni, mingi ya ‘mikosi’ hiyo inatokana na usahaulifu wa kujitakia kwa Wakenya.

Ni kama maradhi ya kujitakia. Ni msiba wa kujitakia ambao hauna kilio.Wakati umefika jamii ianze kujifunza kutokana na makosa iliyofanya awali.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wataka bomba la majitaka likarabatiwe upesi

Nigeria yaondolea Twitter marufuku

T L