• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:50 AM
Nigeria yaondolea Twitter marufuku

Nigeria yaondolea Twitter marufuku

Na MASHIRIKA

ABUJA, NIGERIA

NIGERIA imeondoa marufuku dhidi ya mtandao wa Twitter, miezi saba baada ya kupiga marufuku matumizi ya mtandao huo wa kijamii.

Serikali ya Nigeria ilipiga marufuku matumizi ya mtandao huo Juni 2021, baada yake kufuta ujumbe ulioandikwa na Rais Muhammadu Buhari kuhusu hatua ambazo angeyachukulia makundi yanayayopigania baadhi ya majimbo kujitenga na taifa hilo.

Serikali hiyo iliulaumu mtandao huo kwa kuyaunga mkono makundi hayo.

Lakini Alhamisi, serikali ilisema iko tayari kuondoa marufuku hayo, baada ya Twitter kukubali masharti iliyowekewa, baadhi yakiwa kufungua afisi katika taifa hilo.

Hatua hiyo itawaruhusu mamilioni ya watu katika taifa hilo kuanza kutumia mtandao huo tena.

Hata hivyo, baadhi ya watu bado waliendelea kutumia mtandao huo kupitia mitandao ya intaneti ya kibinafsi.

Serikali hata hivyo iliapa kuwachukulia hatua kali wale ambao walikuwa wakiendelea kuutumia mtandao huo, yakiwemo mashirika ya habari.

Baada ya marufuku hayo, serikali ilikosolewa vikali na jamii ya kimataifa kwa “kuingilia uhuru wa kujieleza.”

Kulingana na Mamlaka ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia (ICT) ya nchi hiyo, hatua ya Twitter kufungua afisi huko “inaonyesha imejitolea kurejesha na kuboresha uhusiano uliokuwa hapo awali.”

Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Kashifu Inuwa Abdullahi, alisema kwenye taarifa kuwa Rais Buhari ametoa maagizo marufuku kuondolewa.

“Twitter imekubali kutathmini upya utendakazi wake kwa kutambua sheria, tamaduni na msingi wa kihistoria wa taifa hili,” akasema Abdullahi.

Alisema mtandao huo “utashirikiana pamoja na serikali hiyo kubuni utaratibu maalum utakaozingatiwa kwenye ushirikiano mpya kati ya pande hizo mbili.”

“Hivyo, serikali ya Nigeria imeondoa marufuku hayo kutoka leo (jana Alhamisi),” akaeleza.

Mkurugenzi huyo alisema Twitter pia imekubali kuzingatia masharti ya ulipaji ushuru kwa taifa hilo.

Hadi sasa, Twitter haijatoa taarifa yoyote kuhusu hatua ya Nigeria kutoa marufuku hayo.

Ilipotangaza marufuku hayo, Nigeria iliwaagiza watu na mashirika yote yanayotoa huduma za mitandao kuufunga mtandao huo.Ilidai mtandao huo “unatumiwa kuvuruga amani na uthabiti wa kisiasa nchini humo kwa kusambaza habari feki ambazo huenda zikawapotosha raia.”

Kwenye ujumbe alioweka katika mtandao huo, Rais Buhari aliapa “kuwakabili watu hao vikali kwa njia ambazo wangeelewa wao wenyewe.”

Alirejelea ukatili ulioshuhudiwa nchini humo kwenye vita vilivyotokea kati ya 1967 na 1970.

Twitter ni miongoni mwa mitandao ya kijamii maarufu sana nchini Nigeria, hasa kuwashinikiza raia kuungana kutekeleza jambo fulani linaloiathiri nchi.Wanaharakati waliutumia kutafuta uungwaji mkono wakati wa maandanano dhidi ya ukatili wa polisi chini ya kaulimbiu #EndSars mwaka 2020.

Kampeni hiyo ilirejelea mauaji yaliyokuwa yakitekelezwa na kikosi maalum cha polisi kilichobuniwa na serikali kukabili uhalifu.

Hata hivyo, maelfu ya raia walilalamikia utendakazi wake, wakisema kilikuwa kikiwalenga watu ambao hawana hatia yoyote.

Mtandao huo pia ulitumiwa pakubwa kuendeleza kampeni ya kuishinikiza serikali kuimarisha juhudi za kuwarejesha karibu wasichana 300 waliotekwa nyara na wapiganaji wa kundi la Boko Haram mwaka 2014.

Kampeni hizo ziliendeshwa na makundi ya kutetea haki za binadamu katika sehemu mbalimbali duniani chini ya kaulimbiu ya #BringBackOurGirls.?Kulingana na takwimu za serikali, karibu watu 40 milioni nchini humo huwa wanatumia mtandao huo.

Amerika, Umoja wa Ulaya (EU) na Canada ni miongoni mwa nchi zilizoungana na wanaharakati kuikosoa Nigeria kutokana na marufuku hayo.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Usahaulifu: Gonjwa hatari sana wanalougua...

Siri ya kufanikisha ufugaji wa kuku hii hapa

T L