• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
WANDERI KAMAU: Wataalamu wetu wafanye bidii kuvumisha Kiswahili

WANDERI KAMAU: Wataalamu wetu wafanye bidii kuvumisha Kiswahili

NA WANDERI KAMAU

MWAKA 2021, Umoja wa Mataifa (UN) ulitenga Julai 7 kila mwaka kuwa Siku ya Kiswahili Duniani.

Tangazo hilo lilitolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwenye kikao kilichofanyika jijini Paris, Ufaransa.

Kikao hicho kilijumuisha mataifa 41 wanachama wa Umoja huo.

Ikiwa ni mwaka mmoja leo tangu kukwezwa kwa Kiswahili kuwa moja ya lugha zinazotambulika, kusherehekewa na kuenziwa duniani, lugha hiyo imepiga hatua kubwa.

Wiki jana, jimbo la British of Columbia nchini Canada, lilipitisha hoja ya kubuni Wiki ya Jamii ya Waswahili—kati ya Julai 2 na Julai 9—kukitambua na kukisherehekea Kiswahili.

Kwenye hoja hiyo, gavana wa jimbo hilo alisema, uamuzi huo unalenga kupiga jeki utambuzi wa Kiswahili kama mojawapo ya lugha zenye ushawishi mkubwa duniani na UN.

Utambuzi huo bila shaka unaashiria ufanisi mkubwa unaoendelea kupatikana kwenye juhudi za kutambua mchango wa Kiswahili duniani. Hata hivyo, juhudi za kukiendeleza Kiswahili katika mataifa ya Afrika bado zimekwama. Hapa nchini, tofauti baina ya wasomi na wadau mbalimbali wa lugha hiyo, ndizo zinatajwa kuchangia kutobuniwa kwa Baraza la Kitaifa la Kiswahili.

Hii ni licha ya Baraza la Mawaziri kupitisha hoja ya kubuniwa kwa baraza hilo mnamo 2018.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Ikulu mara tu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kutia saini hoja hiyo, uamuzi huo “ulilingana na Sehemu 137 ya Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).”

Kipengele hicho kinaihitaji kila nchi ambayo ni mwanachama wa jumuiya hiyo kuwa na baraza la kitaifa la Kiswahili.

Wasomi wengi walisifia sana hatua hiyo, wakiitaja kuwa “mwanzo mpya kwenye juhudi za kukuza Kiswahili nchini.”

Licha ya matumaini yaliyokuwepo, migawanyiko baina ya wasomi, watengenezaji mitaala, taasisi za elimu kati ya wadau wengine bado zingalipo.

Ni kinaya kuwa, wakati mataifa ya kigeni kama vile Canada yanapitisha hoja ya kukitambua Kiswahili na hata kutenga wiki maalum ya kuwaheshimu wazungumzaji wake, sisi bado tunavutana kuhusu mikakati ya kuendeleza lugha hiyo.

Ukweli ni kuwa, kando na kujikosea wenyewe, tunakiuka moja ya kanuni za jumuiya ya EAC.

Kinyume na Kenya, Tanzania imekuwa na Baraza la Kitaifa la Kiswahili (BAKITA). Huu ndio wakati wa wadau wote husika kuondoa tofauti zao, ili Kenya kuanza safari mpya ya ushirikiano kwenye ukuzaji wa Kiswahili.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Magavana wajao watii sheria za ugatuzi kuhusu...

MWANGI MURAYA: Kiko wapi Kiswahili katika manifesto za...

T L