• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 8:00 AM
AK yaitisha mkutano na makocha wakune vichwa jinsi ya kushinda mbio za masafa marefu

AK yaitisha mkutano na makocha wakune vichwa jinsi ya kushinda mbio za masafa marefu

Na AYUMBA AYODI

SHIRIKISHO la Riadha Kenya (AK) limeitisha mkutano na makocha 30 kujadili na kuangalia jinsi Kenya inavyoweza kupata matokeo mazuri katika mbio ndefu kwenye Riadha za Dunia jijini Budapest, Hungary mwezi Agosti 2023.

Mkurugenzi wa mashindano wa AK, Paul Mutwii amefichua kuwa makocha hao hutia makali wanariadha wanaoshiriki mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji, 5,000m na 10,000m. Watakutana katika makao makuu ya AK, Riadha House mnamo Juni 5, 2023.

Mutwii amedokeza kuwa makocha walioitwa katika mkutano huo ni wale ambao wanariadha wao wana nafasi nzuri ya kushiriki Riadha za Dunia zitakazofanyika Agosti 19-27.

Wakati huo huo, AK imekutana na makocha wa wanariadha wanaoshiriki mbio za kilomita 42 watakaopeperusha bendera ya Kenya jijini Budapest kabla ya majina yao kutangazwa.

“Sote tunajua kuwa mambo hayajakuwa mazuri kwetu katika riadha za uwanjani na tunakabiliwa na presha kali sana katika marathon baada ya kukosa medali kwenye Riadha za Dunia jimboni Oregon, Amerika mwaka jana,” amesema Mutwii.

Ameeleza kuwa tayari wamechagua watimkaji wanane wa marathon wanaume na idadi sawa ya wanawake kwa ajili ya mashindano ya Budapest.

“Nakutana nao na makocha wao mjini Eldoret kupata mwelekeo kabla tutangaze timu,” akasema Mutwii.

Kenya haijashinda mbio za wanaume za umbali wa mita 5,000 tangu Benjamin Limo mwaka 2005 jijini Helsinki apate ushindi. Ilikaribia sana mwaka 2007 (Osaka), 2015 (Beijing) na 2022 (Eugene) wakati Eliud Kipchoge,  Caleb Ndiku na Jacob Krop walivunia nchi medali za fedha.

Katika mbio za 5,000m za wanawake, Kenya na Ethiopia zimebadilishana mataji tangu 2003. Kinadada kutoka Kenya wameshinda makala manne nao Waethiopia mara sita.

Hellen Obiri alitawala 5,000m mwaka 2017 jijini London na 2019 jijini Doha kabla ya Muethiopia Gudaf Tsegay kunyakua taji la 2022 mjini Eugene.

Charles Kamathi ni Mkenya wa mwisho kushinda taji la dunia la 10,000m mjini Edmonton, Canada mwaka 2001. Geoffrey Kamworor na Stanley Waithaka walinyakua nishani ya fedha katika makala ya 2015 (Beijing) na 2022 (Eugene), mtawalia.

Kenya bado haijapata taji la mbio za 10,000m upande wa wanawake tangu Vivian Cheruiyot mwaka 2015 jijini Beijing. Cheruiyot alinyakua mataji ya 5,000m na 10,000m mwaka 2011.

Obiri aliridhika na fedha mjini Eugene mwaka 2022 baada ya kulemewa na Muethiopia Letesenbet Gidey.

Utawala wa Kenya wa miaka 15 kama wafalme wa mbio za 3,000m kuruka viunzi na maji pia ulifika kikomo mwaka 2022 baada ya Mmoroko Soufiane El Bakkali kutwaa taji. El Bakkali pia alimaliza utawala wa Kenya wa miaka 38 kwenye Olimpiki wakati wa Olimpiki 2020 jijini Tokyo.

Ethiopia imetawala makala mawili yaliyopita ya marathon ya wanaume kwenye Riadha za Dunia kupitia kwa Lelisa Desisa (2019) na Tamirat Tola (2022).

Kenya ilipoteza taji la dunia la kinadada mwaka 2022 wakati Muethiopia Gotytom Gebreslase aliponyoka nalo. Miaka mitatu kabla ya hapo, Mkenya Ruth Chepng’etich alikuwa ameibuka bingwa wa dunia. Kenya haikuwa imepata taji la kinadada katika makala mawili mfululizo kabla ya ushindi wa Chepng’etich.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

MKU yakariri kujitolea kuendelea kushiriki makongamano ya...

Upande wa mashtaka waomba Mackenzie aendelee kukaa...

T L