• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Ancelotti aweka historia ya kushinda mataji ya ligi katika Ligi Kuu zote tano za bara Ulaya

Ancelotti aweka historia ya kushinda mataji ya ligi katika Ligi Kuu zote tano za bara Ulaya

Na MASHIRIKA

CARLO Ancelotti aliweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kushinda ligi katika ligi kuu tano za bara Ulaya baada ya kuongoza waajiri wake Real Madrid kupepeta Espanyol 4-0 mnamo Jumamosi na kunyanyua taji la Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Mabao mawili kutoka kwa Rodrygo na mengine kutoka kwa Marco Asensio na Karim Benzema yaliwazolea Real taji la 35 katika soka ya La Liga.

Real kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 81 huku pengo la alama 17 likitamalaki kati yao na nambari mbili Sevilla. Zimesalia mechi nne kwa kampeni za La Liga msimu huu kutamatika rasmi.

Ancelotti ambaye ni raia wa Italia, amewahi pia kunyanyua mataji ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A), Ufaransa (Ligue 1), Uingereza (EPL) na Ujerumani (Bundesliga).

Real walishuka ugani kuvaana na Espanyol wakihitaji sare ya aina yoyote ili kutawazwa mabingwa wa La Liga msimu huu. Hata hivyo, Rodrygo aliwafungulia karamu ya mabao katika dakika ya 33 kabla ya kupachika wavuni goli la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kumzidi maarifa beki Sergi Gomez.

Asensio alicheka na nyavu za wageni wao katika dakika ya 55 kabla ya Benzema kujaza kimiani krosi ya Vinicius Jr dakika tisa kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Ancelotti alirejea Uhispania kudhibiti mikoba ya Real kwa awamu ya pili mwishoni mwa msimu uliopita wa 2020-21 baada ya miamba hao kuagana na kocha Zinedine Zidane. Alikatiza uhusiano wake wa miezi 18 na Everton ya EPL.

Ancelotti, 62, aliwahi pia kushinda mataji matano ya haiba katika kipindi cha miaka miwili ya kuhudumu kwake kambini mwa Real katika awamu ya kwanza kati ya 2013 na 2015. Miongoni mwa mataji hayo ni la ‘La Decima’ lililokuwa la 10 kwa Real kujizolea katika soka ya bara Ulaya.

Alitwaa taji lake la kwanza ligini akiwa mkufunzi mnamo 2004 akidhibiti mikoba ya AC Milan, klabu aliyoshindia mataji mawili ya Serie A akiwa mchezaji katika miaka ya 1980.

Alishindia Chelsea taji la EPL mnamo 2010 kabla ya kuongoza Paris Saint-Germain (PSG) kutwaa ubingwa wa Ligue 1 mnamo 2013 kisha kunyanyua ufalme wa Bundesliga akidhibiti mikoba ya Bayern Munich mnamo 2017.

Ancelotti huenda akaongoza Real kukamilisha kampeni za msimu huu wa 2021-22 wakijivunia mataji mawili kabatini mwao. Hiyo ni iwapo watabatilisha kichapo cha 4-3 walichopokezwa na Manchester City ya Uingereza kwenye mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Mei 4, 2022 na kutinga fainali itakayowakutanisha na Liverpool au Villarreal.

Iwapo watatinga fainali ya UEFA na kunyanyua taji la UEFA, basi Ancelotti atakuwa mtu wa pekee kuwahi kushinda taji la European Cup au UEFA mara nne akiwa kocha. Aliwahi kuongoza AC Milan kujizolea ufalme wa kipute hicho mnamo 2003 na 2007.

Fowadi matata raia wa Wales, Gareth Bale ambaye ataagana rasmi na Real mkataba wake ugani Santiago Bernabeu kutamatika msimu huu, hakuwa sehemu ya sherehe za kikosi chake baada ya kupepeta Espanyol na kutwaa taji la La Liga.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, sogora huyo wa zamani wa Tottenham Hotspur alisema: “Yasikitisha kwamba sitakuwa sehemu ya sherehe hizo jioni hii kwa sababu ya jeraha la mgongo linalonitatiza. Hata hivyo, nakionea fahari kikosi cha Real kwa ushindi huo wa taji la La Liga.”

MATOKEO YA LA LIGA (Jumamosi):

Real Madrid 4-0 Espanyol

Alaves 2-1 Villarreal

Valencia 1-1 Levante

Bilbao 2-0 Atletico

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Dortmund wapoteza mechi ya Bundesliga licha ya Haaland...

KIGODA CHA PWANI: Ngoma ya umoja wa kisiasa Pwani imepoa,...

T L