• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
KIGODA CHA PWANI: Ngoma ya umoja wa kisiasa Pwani imepoa, je kunani?

KIGODA CHA PWANI: Ngoma ya umoja wa kisiasa Pwani imepoa, je kunani?

NA BENSON MATHEKA

NI takriban miezi mitatu tu iliyosasalia kabla ya uchaguzi mkuu ujao na suala la umoja wa Pwani lililokuwa vinywani mwa wanasiasa wengi kuanzia mwaka 2021 limesahaulika kabisa.

Wanasiasa wa Pwani walilipigia debe suala la umoja huo kuwepo kabla ya uchaguzi wa Agosti 9 huku wakiwa na uhakika kuwa viongozi wa Pwani wataketi kwenye meza moja na kupigania mgao wa ‘keki’ ya kitaifa kama jamii nyingine kwa pamoja.

Wananchi wengi walidhania wakati huu wa kisiasa, Pwani itakuwa na viongozi wanaopigania haja zao katika kumbi za kitaifa na pia kutoa masharti ambayo yanafaa kutimizwa na wanaowania viti vya kitaifa kwa niaba yao.

Suala la umoja wa Pwani limekuwa kama wimbo kila baada ya miaka mitano kwani wanasiasa hulikumbuka wakati wa uchaguzi huku wakitaka kuchaguliwa.

Ngoma ya kuwepo kwa umoja huo wa Pwani ilionekana kufifia mwanzoni mwa mwaka huu na ilizimwa kabisa baada ya kura ya mchujo ya hivi majuzi ambapo wanasiasa walipewa tikiti na vyama kuwania viti tofauti vya kisiasa.

Kulingana na wachanganuzi wa siasa, wanasiasa ambao hujadili umoja wa pwani kila uchaguzi mkuu unapokaribiapo hudai kuwa muungano wa kisiasa wa jamii za Wapwani ndio unaoweza kuwatoa katika lindi la upweke wa siasa ya kitaifa.

Hata hivyo, baadhi ya wanasiasa hususan wale ambao wako katika vyama visemekanavyo kuwa vya kitaifa nchini huwa wanasema kuwa Pwani haiwezi kusimama peke yake bila ya kujihusisha na wanasiasa wengine nchini.

Wachanganuzi wa siasa wanasema kuwa umoja wa Pwani utazidi kuwa ndoto iwapo mikakati mwafaka inayohusisha wakazi hao haitabuniwa ili kusaidia kuzindua umoja huo.

Chambo

Kulingana na mkazi mmoja wa Malindi aliyejitambulisha kama Abdallah, suala la umoja wa Pwani hutumiwa kama chambo na wanasiasa kupata kura peke yake.

“Kwa nini hatusikii umoja huo kila wakati hata baada ya wao kuchaguliwa? Wacha tubaki vivyo hivyo tu na kuendelea kupangwa,”anasema Abdallah aliyekuwa katika mkao mmoja wa gumzo la siasa eneobunge la Kisauni.

Baadhi ya wachanganuzi wa siasa pia wanasema kuwa tofauti na maeneo mengine nchini ambayo yanaonekana kuwa na umoja wa kisiasa, eneo la pwani lina makabila mengi ndiposa umoja huo unaonekana kuwa hauwezi kutekelezwa.

Bw Mwakera Mwandwamrombo ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa anasema kuwa kutokuwa na umoja wa kisiasa kati ya viongozi wa Pwani, ni jambo ambalo lilianza kabla ya Kenya kupata uhuru na kuendelezwa baadaye kwa sababu ya maslahi ya kibinafsi ya watu.

Kulingana na mchanganuzi huyo wa siasa, baada ya kufariki kwa viongozi kama vile Ronald Ngala, Sharif Nassir na Karisa Maitha ambao walikuwa mbele kuunganisha Wapwani, eneo la Pwani liliachwa bila mwelekeo huku viongozi walioko sasa wakifuata vyama visivyo na asili ya Pwani.

Anaongeza kuwa tofauti za viongozi wa Pwani kuhusiana na umoja wao ndio kuliwafanya wengine kuamua kubaki na vyama walivyonavyo kwa sasa na kufanya umoja huo kutofaulu.

“Kwa kutokuwa na chama cha kisiasa kutetea maslahi ya Wapwani, eneo hili limebaki mikononi mwa wanasiasa wanaoalikwa katika vyama vingine,” alisema Bw Mndwamrombo.

Bw Mndwamrombo anasema kuwa kukosekana kwa umoja wa kisiasa wa Pwani kunafanya hali kuwa tata kwa wanachama wa vyama asilia vya Pwani kama vile Pamoja African Alliance (PAA), Umoja Summit Party, Shirikisho na Kadu Asili ambao watashindana na ‘ndugu’ zao walio katika vyama kama vile ODM, United Democratic Alliance, Jubilee na Wiper.

“Jambo hili linafanya eneo la Pwani kuwa katika njia-panda bila jambo lolote la kujitetea katika meza ya kitaifa na kubaki tu eneo la kujazia kura kwa wanaogombania urais,” akasema Bw Mndwamrombo.

Uongozi bora

Mhadhiri katika chuo kiikuu cha Pwani kilichoko kaunti ya Kilifi, Prof Halimu Shauri anasema kuwa suala la umoja wa Pwani si rahisi kufaulu na litahitaji uongozi bora la sivyo litabakia kuwa wazo tu.

Anasema kuwa changamoto iliyopo kwa sasa ni kufahamu umoja huo unaotakikana ni wa nini kwani kuna watu wanaoangazia masuala yao ya kibinafsi.

“Wengi wanaoongea kuhusu umoja wa siasa ni kuhusiana na maslahi ya watu binafsi na wala sio yale ya wananchi au jamii,” asema Prof Shauri na kuongeza kuwa siasa haiwezi kuwa kigezo kikuu cha umoja wa Pwani bali itakuwa kama chombo cha kuhamasisha kuhusu suala hilo.

Anaendelea kuwa viongozi wa zamani waliopendekeza umoja wa Pwani walikuwa na malengo mazuri na walionekana kujiondoa wakati tu suala hilo lilipoingiliwa na wanasiasa,Prof Shauri anasema pia vyama vyenye asili ya Pwani haviwezi kuendesha ajenda ya umoja wa Pwani kwani vina maslahi yanayotofautiana.

Mwaka 2021, katika mkutano wa chama cha PAA, Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi alisema kuwa kila kona ya nchi watu wanajipanga na kwamba wakati wa eneo la Pwani wa kujipanga ni sasa.

“Tumezoea kupangwa, wakati sasa umefika tujipange sisi wenyewe,” akanukuliwa Bw Kingi katika mkutano huo.

Kwa sasa chama cha PAA kiliweka makubaliano ya ushirikiano na chama cha Jubilee na kiko chini ya mwavuli wa chama cha Azimio la Umoja One-Kenya ambacho mgombea wake wa urais ni Bw Raila Odinga.

Baadhi ya viongozi wa Pwani walio katika chama cha chama Azimio kupitia vyama vyao ni Gavana wa Mombasa, Hassan Joho, mbuge wa Mvita, Abdulswamad Nassir na mbuge wa Likoni, Mishi Mboko.

Walio katika muungano wa Kenya Kwanza Alliance kupitia vyama vyao ni pamoja na Gavana wa Kwale, Salim Mvurya na naibu wake Fatuma Achani, seneta wa zamani wa Mombasa, Bw Hassan Omar anayewania ugavana wa Mombasa na mbuge wa Nyali, Mohamed Ali.

Kwa sasa wakazi wa Pwani wanasubiri miaka mingine mitano baada ya uchaguzi ujao ili kuanza kusikia tena ngoma ya umoja wa Pwani ikirindima.

  • Tags

You can share this post!

Ancelotti aweka historia ya kushinda mataji ya ligi katika...

Wakenya watawala Pittsburgh Half Marathon

T L